Tanzania Prisons sasa imezaliwa upya

Saturday February 9 2019

 

By OLIPA ASSA

KOCHA wa Prisons, Mohamed ‘Adolf’ Rishard amepindua meza baada ya kukaa kwa muda mrefu mkiani na kuisaidia timu hiyo kushika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Tangu ajiunge na timu hiyo akipokea mikoba ya Mohamed Abdallah ‘Bares’, Prisons imekuwa na mabadiliko na imeshinda mechi tofauti na awali ambapo ilikuwa inaambulia sare.

Mpaka sasa Prisons, imecheza mechi 24 imeshinda nne, sare 11 na imefungwa tisa na kukusanya pointi 23, jambo ambalo Kocha Adolf alisema linampa faraja.

“Ligi ni ngumu lakini kazi yetu ni kupambana kama wenzetu wanavyotimiza malengo yao. Ndio tumeanza naamini tutakuwa na mwisho mzuri.

“Mzunguko wa pili unamchanganya kila kocha na kumuumiza kichwa ili amalize kishujaa. Naendelea kuzungumza na wachezaji wangu wajitume,” alisema.

Mechi ya mwisho Prisons ilicheza dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuiibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Advertisement