Tajiri Yanga apagawisha mastaa

KITENDO cha mdhamini wa Yanga, GSM kuibuka mazoezini kwenye Uwanja wa Shule ya Sheria juzi Ijumaa jioni kilishtua mastaa wa timu hiyo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hersi Said ambaye wachezaji wengi wamezowea kukutana naye ofisini wakati wa makubaliano ya mikataba walishtuka baada ya kumuona laivu uwanjani akishuhudia mazoezi hayo.

Mwanaspoti ambalo lilikuwepo uwanjani hapo lilishuhudia wachezaji wakiwa na mzuka wa aina yake baada ya kugundua kwamba nje alikuwa amekaa mwakilishi wa GSM, Hersi na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Mshindo Msolla.

Viongozi hao walifuatilia muda wote mazoezi ya vijana wao kuanzia mwanzo mpaka mwisho ambapo kocha wao msaidizi, Charles Mkwasa alikuwa akifanya mambo yake ndani ya uwanja.

Baada ya kumaliza wachezaji walikusanywa sehemu moja na ndipo Msolla alimuita Hersi kisha kumpa muda wa kuzungumza na wachezaji hao kikao ambacho kilichukua takribani dakika 10.

Hersi alitumia dakika hizo kuwaambia wachezaji kwamba wako pamoja nao kwenye kila jambo wanalofanya ndani na nje ya uwanja na lengo ni kuona Yanga inafanikiwa zaidi.

Aliwaambia kwamba anachotamani kwa muda huu uliobaki ni kuona Yanga inamaliza kwa kishindo mechi zake zilizobaki na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, lakini nguvu yao kubwa waelekeze kwenye Kombe la FA.

Mwanaspoti lilishuhudia akiwasisitiza kwamba atawasaidia kwa kila hali ili kuhakikisha kwamba wanatwaa ubingwa wa FA na kushiriki michuano ya kimataifa mwakani kwani ndio wamepanga kuongeza nguvu kubwa kwenye usajili.

Baada ya kumaliza kikao na wachezaji hao walimshukuru na kunyanyuka kuondoka na kuwaacha viongozi na benchi la ufundi wakiyajenga mpaka giza lilipoingia, ambapo katika kikao hicho Mkwassa alielezea maendeleo ya mazoezi na mikakati yake huku uongozi ukimueleza mambo mbalimbali ikiwemo usajili mpya ambao waliwaambia kila kitu kinaendelea vizuri.

Walipoanza kutawanyika Mwanaspoti liliwafuata Dk Msolla na Mkwassa kuweza kupata majumuisho ya kile walichozungumza lakini wakakausha kwa madai kwamba zilikuwa ni ishu zao za mikakati ya ndani.

Mmoja wa vigogo wa Yanga alidokeza kwamba GSM imewasisitiza kuwa mapambano yameanza kwenye ligi na Kombe la FA, hivyo kila mmoja aongeze juhudi kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na mikakati inatimia kwa wakati.

Mmoja wa mastaa wa Yanga alidokeza kwamba tajiri huyo aliwaambia wajitahidi kumaliza ligi kwa heshima ya nafasi ya pili, lakini akili yao yote waiweke kwenye FA ambako ndiko kuna nafasi ya kushiriki kimataifa mwakani na yeye atawasapoti.

Yanga inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 51 katika michezo 27 waliyocheza huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Azam FC waliocheza mechi 28 na kupata pointi 54.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael ambaye bado yupo kwao Ubelgiji amesisitiza kwamba mpango wao ni kutwaa kombe la FA kwa vile mastaa wengi wakubwa anaowasajili msimu ujao akili yao ipo kimataifa zaidi na ndiko walikozowea.

Aliongeza kuwa kama wakiikosa nafasi hiyo watalazimika kutumia nguvu za ziada ikiwemo fedha kuwashawishi wachezaji hao kusaini kujiunga na Yanga kwani kwenye klabu zao walishazowea kila msimu kucheza michuano ya kimataifa na sio tu ligi za ndani.