TP Lindanda wawapigia hesabu za ushindi Wajeda FDL

Muktasari:

Ni mchezo wa Daraja la Kwanza utakaopigwa Uwanja wa Nyamagana ambapo Pamba wako nafasi ya nane na pointi 25 huku Mashujaa akiwa wa sita na alama 27.

PATACHIMBIKA, Pamba FC itakuwa na kazi nzito pale itakapowaalika Mashujaa katika pambano la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) litakalopigwa Uwanja wa Nyamagana jijini hapa kesho Jumamosi..

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma,Mashujaa ilishinda 2-0.

 Pamba wako nafasi ya nane na pointi 25 huku wapinzani wao wakiwa wa sita na alama 27 ambapo Gwambina anaongoza kundi hilo B na pointi 44 ambapo tayari wameshapanda Ligi Kuu.

 Mchezo huo utakuwa na upinzani mkali kwani Pamba wakipoteza watakuwa wamejiweka katika nafasi mbaya ya kushuka daraja huko Mashujaa wakihitaji ushindi ambao utawafanya wawe sehemu nzuri ya kucheza hatua ya  mtoani wa kupanda Ligi Kuu.

 Akizungumza na Mwanaspoti Online, Nahodha wa Pamba, Alex Mwaisaka alisema wanajua umuhimu wa mchezo huo hivyo wataingia kwa tahadhari kubwa ili kuweza kuondoka na pointi tatu.

 "Ni mchezo ambao kama tukipoteza basi tutakuwa katika nafasi mbaya ya kushuka daraja hivyo tunajua umuhimu wake na tumejipanga kuwakabili Mashujaa," alisema.

 "Tunataka kwenye hizi mechi mbili zilizobaki tuweze kupata pointi sita ambazo zitatufanya tufikishe alama 31 ambazo zitatuweka katika nafasi nzuri ya kubaki daraja msimu ujao," alisema Mwaisaka.

 Nahodha wa Mashujaa,Abdalah Juma alisema wanajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika pambano hilo.

 "Hii mechi kwetu ni kama fainali kwani tunataka tupate ushindi ambao utatuweka katika nafasi nzuri kwenye mchuano wa kusaka kucheza Ligi ya mchujo," alisema Juma.