TFF yamtupia virago kocha Mirambo wa Serengeti Boys

Wednesday June 12 2019

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam.Baada ya kufanya vibaya katika mashindano ya Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, (Afcon), Shirikisho la Soka Tanzania limetangaza kumtimua kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo.

Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kufanya vibaya kwa timu ya Serengeti Boys kumechangia kuvunja benchi la ufundi lote la timu hiyo.

Karia alisema kocha mkuu wa Serengeti Boys, Mirambo na benchi lote la ufundi wataondolewa katika nafasi hiyo.

"Tutamtafuta kocha mwingine wa kuziba nafasi hiyo, baada ya Mirambo kushindwa kuisaidia Serengeti Boys kufanya vizuri katika mashindano ya Afcon hapa nyumbani," alisema.

"Tunaomba radhi kwa Watanzania wote kutokana na matokeo mabaya tuliyoyapata katika mashindano hayo tumejifunza mambo mengi," alisema Karia.

Katika mashindano ya Afcon U17, Tanzania ilitolewa katika hatua ya makundi baada ya kufungwa mechi zote ikifungwa 5-4 na Nigeria, ikachapwa 3-0 na Uganda na kumaliza kwa kipigo cha mabao 4-2 na Angola.

Advertisement

Advertisement