TFF wajificha na Morrison

LICHA ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuahidi kushughulikia malalamiko ya Yanga jana juu ya uhalali wa mkataba wa mchezaji Bernard Morrison na Simba, Yanga wenyewe wametamka kwamba; “Tumeachana na hilo shauri.”

Katibu Mkuu wa Yanga, Simon Patrick aliiambia Mwanaspoti jana kwa kifupi kwamba wameachana na shauri hilo lakini Ofisa Habari wa Yanga akaendelea kusisitiza kwamba walipeleka malalamiko na wanasubiri uamuzi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye ni Mwanasheria kitaaluma, Elias Mwanjala licha ya kukutana jana haikuweza kutoa ufafanuzi wowote juu ya sakata la mchezaji huyo ambaye katika miezi ya hivi karibuni amekuwa gumzo nchini.

Jana wajumbe wa kamati hiyo, walikutana nyakati za mchana katika Makao Makuu ya TFF, Karume jijini na kufanya kikao kilichochukua muda mrefu kumalizika ambacho hata hivyo taarifa ya kikao hicho haikutolewa kwa maelezo kuwa ni cha ndani lakini mmoja wao akasema; “Ishu ya Morrison haikuwepo.”

“Ni kweli tumekutana lakini suala la Morrison halikuwepo na wala hatukulijadili,” alidai mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo huku akiingia kwenye gari lake na kuondoka.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Elias Mwanjala alisema kuwa iwapo jambo hilo lingewasilishwa mbele ya kamati yake, wangelijadili na kulitolea uamuzi kwa haraka.

“Sijajua ajenda zitakuwa zipi hadi nifike kwenye kikao, lakini kama ishu ya Morrison itakuwa imeletwa pia tutaijadili na kuitolea ufafanuzi.

“Ishu ya madai ya Yanga juu ya uhalali wa mkataba wa mchezaji huyo na Simba nimeisikia tu kwenye vyombo vya habari, ila kama itakuwa imeletwa mezani kwetu katika kikao, basi tutaijadili na kuimaliza kwa haraka,” alisisitiza Mwanjala kabla ya kikao cha jana ingawa baadaye alipopigiwa simu hakutoa ushirikiano.

Sakata la mkataba wa Morrison liliibuka upya hivi karibuni baada ya Yanga kudai mkataba ambao mchezaji huyo alisaini kuitumikia Simba ulikuwa na upungufu.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema mkataba huo haukuwa na saini ya klabu ya Simba zaidi ya ile ya mchezaji.

Awali, Morrison ambaye alimaliza mkataba wake wa miezi sita na Yanga, aliingia kwenye mgogoro na klabu hiyo ambayo ilidai imemuongezea mkataba wa miaka miwili huku yeye akipinga kuwa hajaongeza nayo mkataba.

Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, ilieleza kuwa Morrison ni mchezaji huru na akatua Simba.