TBF, fimbo ya mpira wa kikapu Tanzania bado mnayo, mjue

Muktasari:

Huku alipatikana Hasheem Thabeet kwenye NBA kabla ya Mbwana Samatta wa soka kufika Genk na sasa akielekea kushiriki klabu bingwa barani Ulaya.

Tazama ramani utaona nchi nzuri/ Yenye mito na mabonde mengi ya nafaka/ Nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri/ Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzaniaaaaaaaaaa/ Majira yetu haya, yangekuwaje sasa/ Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha... Hiki ni kiitikio cha wimbo bora kabisa unaozungumza hali ya Tanzania na uzuri wake na namna tulivyobarikiwa. Lugha ya mwandishi naamini ililenga kuhakikisha kila anayeisikia anahakikisha kuiendeleza Tanzania iliyomlea na kuwafanya wageni kutambua uzalendo wetu na nia ya kuifanya Tanzania kuwa yenye utofauti na iliyobarikiwa ikiwa ni pamoja na watu wake.

Pamoja na nyimbo hii, lakini sio kila kitu kimekuwa kikienda “smooth” kama wasemavyo wenzetu. Sio kila jambo limekuwa na sura ya umashuhuri wa Tanzania yetu. Ramani yetu ya Taifa ina uzuri tofauti na ramani yetu ya michezo. Moja ya maeneo ambayo tulitakiwa kuwa mbali mpaka sasa ilitakiwa kuwa ni mchezo wa mpira wa kikapu.

Huku alipatikana Hasheem Thabeet kwenye NBA kabla ya Mbwana Samatta wa soka kufika Genk na sasa akielekea kushiriki klabu bingwa barani Ulaya.

Huku kulitakiwa kuwe ni mchezo wa asali na maziwa nchini lakini badala yake umekuwa mchezo wa machozi, jasho na damu. Hakuna urahisi na haionekani kuwepo kwa siku yoyote karibuni hususani katika mazingira ambayo timu ya Taifa inakwama kuishi katika nchi jirani ya Uganda ambako inakuwa imekwenda kushiriki mashindano ya kimataifa.

Ni matatizo ambayo yamelelewa kwa muda mrefu, yameishi na yamezaa “kansa” ambayo inaonekana madaktari ambao ni viongozi waliochaguliwa wamekosa namna ya kusaidia kuokoa mgonjwa huyu ambaye aliwahi kuonekana kuwa ni baraka ambayo iliwahi kuwaleta nchini nyota kama Stephen Curry, Dwight Howard na hata mwaka huu alikuwepo mchezaji Malcolm Brodgon. Pengine ujio wa Rais wa Toronto Raptors, Masai Ujiri na programu yake ya Giant Of Africa inaweza kuwatoa wengi usingizini, basi na waamke.

Kumekuwa na maneno ya kukosekana kwa upendo na ushirikiano baina ya viongozi. Hilo la kwanza halina maana kubwa lakini hili la pili ni muhimu mno kwa shirikisho na wadau wake. Inapotokea wadau wakuu wa mchezo husika wanapoteza imani maana yake ni kuwa hata fimbo ya Mussa haiwezi tena kuwa na maana atakapotaka kupiga maji yagawanyike ili wadau wapite kwenda ng’ambo ya pili.

Ni muhimu kuona Phares Magesa kama Rais wa Shirikisho, Okare na mkoa wa Dar Es Salaam wakizungumza lugha moja na Karabani mdau anayepigania mchezo huu. Sio lazima wapendane lakini ni muhimu washirikiane na watunge lugha itakayowafanya wawe na mazungumzo yatakayoeleweka kwa wenye mchezo wao ambao ni wachezaji, wengi wao wakiwa vijana ambao “YouTube” inawasukuma kuamini NBA panafikika na pia wanafikiwa na Masai Ujiri, Rais wa Toronto Raptors anayewaeleza wawekeze kwenye vipaji vyao.

Tanzania ni ramani inayovutia lakini kwenye michezo haya yapo kwenye maandishi, yapo kwenye taarifa kwenda kwenye vyombo vya habari. Ramani yetu haivutii kuanzia kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa unaovuja maji, haivutii kwenye mipango ya kupitisha bakuli la michango ya timu ya taifa wiki moja kabla ya mashindano. Kwa nguvu moja lazima shirikisho lirudi mezani, liweke mipango na kutafuta washirika ambao wanaweza kuwasaidia kusuka mipango inayoweza kuwa na tija kwa mchezo huu.

Kiongozi mmoja alisikika akiomba hisani ya kujengewa uwanja na wageni wakati Masai Ujiri akiwa Tanzania, lakini jibu la Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete lilikuwa na maana kubwa. Nikimnukuu alisema “haiwezekani tumekuwepo hapa miaka yote na bado tunategemea mtu kutoka nje aje kutusaidia kuanzisha na kusukuma kitu kisonge mbele. Lazima ianzie kwetu, lazima tuwe na tamaa ya kuwa na uwanja wa kisasa. Ni muhimu tuanzishe kitu na ndio tuwaze kupata mwingine wa kutusaidia.”

Miaka takribani miwili iliyopita uongozi wa sasa ulipewa fimbo ya baraka, ulikabidhiwa waumini sisi watufikishe kwenye nchi ya ahadi. Tuliwakabidhi imani yetu pia na fikra zetu zilikuwa zinatuonyesha Tanzania itakayosogea mbele. Hatujawakatia tamaa au pengine wapo waliokata tamaa lakini fimbo bado mnayo. Kuna wimbi la maji mbele, tunategemea kuvuka salama miaka iliyobaki hivyo mpige vyema maji yagawanyike. Ushirikiano utapatikana kwenye uwazi, ushirikiano na uwajibikaji, fungueni roho.