Sven atoa kauli ya kushtua

Sunday October 25 2020
sven pic

LICHA timu nyingi za Ligi Kuu kujawa na hofu kila zinapokutana na fowadi ya Simba iliyotimia, Kocha Sven Vandenbroeck ametamka jambo la kushtua kidogo. Anasema hajaona kile ambacho anahitaji kwa mastraika wake. Sven alisema katika kikosi chake wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini wanatumia chache na kama wangekuwa wakizitumia basi wangekuwa na mabao 14, ambayo wamefunga katika michezo sita ya ligi.

“Ukiangalia mechi na Mlandege, Mugalu alifunga mabao mawili lakini alikosa nafasi nyingi za wazi ambazo angekuwa makini, alikuwa na nafasi ya kufunga zaidi ya hayo na kuongeza akaunti yake ya mabao ambayo yangekuwa faida kwetu.

“Ukifuatilia mechi zetu zote hilo limekuwa likitusumbua tangu mwanzo wa msimu na si kwa Mugalu pekee bali hata Meddie Kagere, John Bocco na Charles Ilanfia na tunalifanyia kazi katika mazoezi yetu ili kubadilika na kufanya vile ambavyo nahitaji kutoka kwao kwenye mechi michezo ijayo. Kagere katika mechi sita amefunga mabao manne, Mugalu amefunga mabao saba katika michezo yote na Bocco amefunga matatu ukilinganisha mechi na mabao waliyofunga yanawabeba, lakini kwangu nina imani wanaweza kuwa bora zaidi ya hapo kutokana na nafasi za kufunga ambazo tunapata.

“Bado nategemea kuwaona mastraika wangu wote wanne, Mugalu, Kagere, Bocco na Ilanfya wanafunga zaidi kutokana na nafasi ambazo tunatengeneza ingawa si jambo baya kwa wengine wakifunga kwani yote yanakwenda kuisaidia kupata pointi tatu,” alisema Sven.

Katika mechi iliyopita na Simba waliocheza na Tanzania Prison iliwakosa Bocco, Kagere na Mugalu na nafasi yao alikwenda kucheza Ilanfia, ambaye alipata nafasi mbili za kufunga ila alishindwa kufanya hivyo.

Kikosi hiko cha Simba jana kilifanya mazoezi kujiandaa na Ruvu Shooting hapo kesho kwenye Uwanja wa Uhuru na Mugalu alikuwa miongoni mwa wachezaji hao.

Advertisement

Wakati Sven akionekana kutokuridhishwa na kasi ya mastraika wake kupachika mabao kutokana na nafasi wanazotengeneza, Mugalu aliliambia Mwanaspoti kuwa kila mechi ambayo atapewa nafasi ya kucheza anatamani kufunga mabao tu.

“Kila mechi huwa napenda kufunga na nispofanya hivyo, huwa naumia na kama ikitokea nimefunga bao moja basi natamani kufunga zaidi,” alisema Mugalu na kuongezea kuwa msimu huu atafunga mabao mengi.

 

Advertisement