Sura za kazi Ulaya

LONDON ENGLAND. HIZI sura weka mbali na watoto. Ndio hivyo maana hakuna wanachofahamu zaidi ya kukuachia tu maumivu unapokutana nao. Hii tunazungumzia safu za washambuliaji watatu wanaotisha kwenye Ligi Kuu za kibabe huko Ulaya.

Unaambiwa hivi, cheza na timu zote, lakini usithubutu kukutwa na fowadi za wababe hawa Barcelona, Liverpool, Manchester City na Paris Saint-Germain. Ukikutana na fowadi za timu hizo na hawajakuachia maumivu makali, basi utakuwa mwenye bahati kwelikweli. Aston Villa usiku wa juzi Jumapili wakiwa nyumbani Villa Park walikutana na shida kubwa walipowakaribisha Manchester City uwanjani kwao katika mchezo wa Ligi Kuu England. Kwenye mchezo huo, kipa wa Aston Villa aliokota mipira mara sita kwenye wavu wake, straika Sergio Aguero akiongoza mauaji hayo makubwa kwa kupiga hat-trick na kuvunja rekodi ya kuwa mchezaji wa kigeni aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu England.

Kwa kifupi tu, kuna sura hizo omba usikutane nazo. Pale PSG kuna Kylian Mbappe, Neymar na Mauro Icardi. Watatu hao kwenye mechi za ligi walizocheza hadi sasa msimu huu, wamehusika kwenye mabao 40. Kwa ujumla, PSG imefunga mabao 46, hiyo ina maana wachezaji wengine walihusika kwenye mabao sita tu. Kwenye mchanganuo wa mabao hayo, Mbappe amefunga 11 na kuasisti manne, Neymar amefunga 10 na kuasisti manne na Icardi amefunga tisa na kuasisti mawili.

Sura nyingine za kutisha kukutana nazo zipo huko Anfield. Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino ni balaa kubwa wakimfanya kocha Jurgen Klopp kupiga tu miluzi kwa kujitanua. Wakali hao wa Liverpool wamehusika kwenye mabao 43 pia katika ligi, huku timu yao ikiwa imefunga mara 50. Ina maana ni mabao saba tu ndiyo yasiyowahusu wakali hao. Mo Salah amefunga 10 na kuasisti tano, Mane amefunga 11 na kuasisti sita na Firmino amefunga mara saba na asisti nne.

Huko Nou Camp kuna sura za mtu tatu, Antoine Griezmann, Luis Suarez na baba lao, Lionel Messi. Wakali hao wamepafanya Nou Camp kuwa mahali pabaya kwa timu za upinzani kwenye mchakamchaka wa La Liga. Sura hizo zimehusika kwenye mabao 48, ambapo Messi amefunga 13 na kuasisti sita, Griezmann mabao saba na kuasisti manne, wakati Suarez ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa msimu wote amefunga 11 na kuasisti saba. Kwa ujumla kwenye La Liga, Barca msimu huu imefunga mabao 49, hivyo ni bao moja tu ndilo ambalo wakali hao hawajahusika.

Pep Guardiola mambo yake ni shwari huko Man City. Kipigo alichowashushia Aston Villa ni mwendelezo tu wa makali wanayotoa mastaa wake kwenye sehemu ya ushambuliaji ambayo imekuwa moto na simulizi ya kutisha kwa mabeki wa timu pinzani. Kwenye fowadi ya timu hiyo, utakutana na sura za wakali hawa moto, Aguero, Raheem Sterling na Gabriel Jesus. Wakati hao wamehusika kwenye mabao 40, huku chama lao la Man City likifunga mabao 62 kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Hiyo ina maana ni mabao 22 tu ndio sura hizo hazijahusika.

Aguero amefunga mabao 13 na kuasisti matatu, Sterling amefunga 11 na kuasisti mara moja, wakati Jesus amefunga tisa na kuasisti mara tatu. Timu hizo zote zimetinga kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu ambapo mchakamchaka wake utaendelea tena mwezi ujao.