Sura za kazi Arsenal, Man United

Thursday January 10 2019

 

LONDON, ENGLAND. JANUARI inakwenda kasi na kijasho kinawatoka makocha Unai Emery na Ole Gunnar Solskjaer katika kusaka wakali wa kuwaingiza kwenye vikosi vyao.

Makocha wote, Emery wa Arsenal na Solskjaer wa Manchester United kila mmoja ana shida kwenye kikosi chake, akitaka kuongeza wakali wapya ili kumaliza msimu vizuri wakipambania kuwamo ndani ya Top Four kwenye Ligi Kuu England.

Emery anataka mabeki na washambuliaji, hivyo ndivyo ilivyo pia kwa Solskjaer huko Old Trafford.

Lakini kila kocha anajaribu kutazama kipaumbele chake, ambapo Emery kwa sasa anataka kuongeza kasi kwenye fowadi yake, wakati Solskjaer anafikiria kuboresha kwenye safu yake ya mabeki.

Makocha hao wawili timu zao zitakutana kwenye raundi inayofuata ya Kombe la FA, ambapo mechi hizo zitakazofanyika kati ya Januari 25 hadi Januari 28, huenda kwenye vikosi vya Arsenal na Man United zitakapokutana Emirates kutakuwa na sura mpya kadhaa kwenye mechi hiyo kama zitasajiliwa kwenye dirisha hili la Januari.

Kocha Emery kwenye orodha yake kuna vichwa vitano vya wachezaji wanaocheza kwenye eneo la ushambuliaji, ambao huenda mmoja wao au hata wawili wakatua kwenye kikosi hicho cha Emirates. Wachezaji hao wa kwanza ni Denis Suarez wa Barcelona. Wengine ambao wapo kwenye rada za Emery ni Malcom, Ousmane Dembele na Isco, huku pia kwenye orodha hiyo akiwamo, Jack Grealish.

Anachotaka Emery ni kutengeneza safu ya ushambuliaji yenye makali ya wembe, ukiuchezea tu, umekatwa. Kwa upande wa Solskjaer, yeye mpango wake ni kunasa mabeki tu na ndio maana amekuwa akihusishwa na mabeki wengi kwenye dirisha hili la Januari.

Anachohitaji kocha huyo wa muda ni kutengeneza ukuta wa zege huko Old Trafford.

Mabeki kibao wanahusishwa na mpango wa kutua Man United kwenye dirisha hili, lakini watatu baina yao ni Eder Militao, Kostas Manolas na Nikola Milenkovic. Hapo hujawaweka kwenye orodha hiyo, Harry Maguire na Diego Godin, ambao wanaweza kunaswa na wababe hao kwenye dirisha hili la Januari. Hizi ndizo sura zinazotajwa huenda zikahusika kwenye mechi ijayo itakayozikutanisha Arsenal na Manchester United.

Advertisement