Suarez azigonganisha Barcelona, Chelsea na Arsenal huko Ulaya

Monday January 14 2019

 

BARCELONA, HISPANIA .HII inaitwa mwenye kupata apate. Arsenal bado inakaza kwenye mpango wake wa kumnasa staa wa Barcelona, Denis Suarez kwenye dirisha hili la Januari, lakini katikati ya mpango huo kuna Chelsea nayo imejipenyeza.

Kocha Unai Emery ameweka wazi anamtaka mchezaji huyo kwenye kikosi chake, hata kama ni kwa mkopo. Lakini, Barcelona nayo inasema haitaki Suarez aondoke kwenye dirisha hili la Januari.

Hata hivyo, kila kitu kinaweza kuwa tofauti ndani ya dirisha hili la Januari kama tu Barcelona itapata mshambuliaji inayemhitaji katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya baridi huko Ulaya. Kwenye orodha ya washambuliaji inayowataka Barcelona, mmoja wao ni Alvaro Morata wa Chelsea.

Na hapo ndipo panapowafanya Chelsea kuingia kati kwenye dili la Suarez. Barcelona inamtaka kwa mkopo Morata, lakini Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri, naye anahitaji kiungo wa kuchukua mikoba ya Cesc Fabregas, hivyo linaweza kufanyika kwa dili la kubadilishana wachezaji, Morata akatua Nou Camp na Suarez akaenda zake Stamford Bridge.

Arsenal inafahamu hilo, hivyo haitaki kujiondoa kwenye mchakato kirahisi hasa baada ya kutambua Suarez mwenyewe anataka kwenda Emirates, kwa sababu anafahamu ni mahali atakokwenda kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.

Arsenal inamtaka Suarez kwa mkopo kwa sasa kwa makubaliano ya kumbeba jumla kwa Pauni 18 milioni mwishoni mwa msimu.

Barca nayo haina shida, itamwaachia Suarez kama tu itampata mshambuliaji mpya kwenye dirisha hili la Januari. Mastaa inaowataka ukimwaacha Morata mwingine ni Fernando Llorente.

Lakini, kubwa ni ishu ya usajili wa Suarez, ambayo imezibananisha pamoja klabu tatu vigogo huko Ulaya, Barcelona, Arsenal na Chelsea. Mwisho utakuwaje, ni suala la kusubiri na kuona.

Wakati huohuo, Barca italazimika kuiandikia hundi ya Euro 800,000 Manchester City baada ya kumtumia Suarez kwenye mechi ya Copa del Rey.

Hayo ni makubaliano yaliyowekwa baina ya timu hizo mbili, kwamba kama kila baada ya mechi 10 atakazocheza, Denis Suarez kwenye kikosi cha Barcelona, basi Manchester City lazima ilipwe mzigo huo.

Mechi hiyo dhidi ya Levante ilikuwa ya 70 tangu Suarez alipohama Manchester City, hiyo ina maana ada yake sasa imefikia jumla ya Euro 7.4 milioni.

Advertisement