Straika Mrundi apania makubwa Mwadui FC

Friday October 12 2018

 

By SADDAM SADICK

Mwanza. Mshambuliaji wa Mwadui, Ibrahim Nasser amesema amepata nguvu mpya ya kuhakikisha anafunga mabao mengi na kuisadia timu yake kujinasua mkiani.

Mwadui imecheza mechi nane na kushinda moja dhidi ya Biashara United ikiwa mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Nasser alisema baada ya kucheza mechi saba bila ya kufunga amefurahi kufunga bao la kwanza katika mechi ya nane dhidi ya Biashara United.

Alisema licha ya kuwa nafurahia kuondoa gundu katika mguu wake, lakini furaha kubwa ni kuipa ushindi wa kwanza timu yake ambayo tangu Ligi ianze walikuwa hawajapata pointi tatu.

“Kwanza ni kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufunga bao, lakini nimefurahi kwa kuipa ushindi wa kwanza timu yangu tangu kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu, niseme nitapambana kuhakikisha nafunga mabao mengi,”alisema Nasser.

Straika huyo Mrundi alisema alichobaini katika Ligi ya Tanzania, timu inayokuwa katika uwanja wa nyumbani ina nafasi kubwa ya kushinda tofauti na nchini kwao.

“Kwanza mabeki wa huku wanatumia nguvu sana kuzuia, pia timu inapokuwa nyumbani inakuwa nafasi kubwa ya kushinda, lakini kwa ujumla tutapambana bila kujali uwanja tunaocheza”alisema Nyota huyo.

Hadi sasa Mwadui ipo mkiani ikiwa na pointi tano baada ya kushuka uwanjani mara nane, huku safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao sita na kufungwa 10.

Advertisement