Sterling mkwanja atakaolipwa Man City tema mate chini

Muktasari:

Ripoti zinadai kwamba makubaliano ya awali baina ya mkurugenzi wa soka wa Man City, Txiki Begiristain, ofisa mratibu mkuu, Omar Berrada na wakala wa Sterling, Aidy Ward Jumatatu, staa huyo Mwingereza sasa atalipwa Pauni 450,000 kwa wiki kwenye dili hilo mpya kama litafikiwa makubaliano.

MANCHESTER, ENGLAND . MANCHESTER City wapo kwenye mazungumzo ya kumfanya staa wao Raheem Sterling kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kuliko wote kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Etihad baada ya kuonyesha kiwango bora uwanjani.

Wakati kwa sasa ikielezwa kwamba winga huyo Mwingereza akilipwa Pauni 300,000 kwa wiki kutoka kwenye dili lake lile alilokubali mwaka mmoja uliopita ambalo linamfanya kubaki kwenye timu hiyo hadi 2023.

Katika kipindi hicho, Sterling alikuwa akishika namba mbili kwa mastaa wanaolipwa pesa nyingi kwenye kikosi cha Man City, nyuma ya kiungo mshambuliaji wa Kibelgiji, Kevin De Bruyne, anayelipwa Pauni 350,000 kwa wiki baada ya kusaini mkataba mpya wa miaka sita Januari 2018.

Ripoti zinadai kwamba makubaliano ya awali baina ya mkurugenzi wa soka wa Man City, Txiki Begiristain, ofisa mratibu mkuu, Omar Berrada na wakala wa Sterling, Aidy Ward Jumatatu, staa huyo Mwingereza sasa atalipwa Pauni 450,000 kwa wiki kwenye dili hilo mpya kama litafikiwa makubaliano.

Man City wanaonekana kusumbuka na namna Real Madrid inavyomtaka staa wake huyo, hivyo katika kumtuliza Etihad wanaona ni vyema kumpa dili hilo jipya lenye mkwanja wa mana. Mastaa wengine wanaolipwa kibosi kwenye kikosi hicho ni Sergio Aguero na David Silva wanaolipokea kwa wiki Pauni 230,000 na 220,000 mtawalia.

Kiungo veterani Fernandinho anaondoka nyumbani na Pauni 150,000 kwa wiki sawa na anavyolipwa Mreno, Bernardo Silva.

Ilkay Gundogan, Rodri, Aymeric Laporte, Riyad Mahrez, Nicolas Otamendi, Kyle Walker na John Stones ni mastaa wengine ambao mishahara yao ina tarakimu sita.