Staa Sancho amwagia sifa Rashford

Monday September 28 2020
sancho pic

DORTMUND UJERUMANI. JADON Sancho, staa anayewindwa na Manchester United, amemmwagia sifa mchezaji mwenzake wa timu ya Taifa ya England anayeichezea miamba hiyo ya Old Trafford, Marcus Rashford kwamba ni mmoja kati ya wachezaji wenye uwezo mkubwa aliowahi kucheza nao.

Inaelezwa, Man United inatarajia kufanya jaribio la mwisho la kumsainisha Sancho kabla ya Oktoba 5, ambapo dirisha la usajili litakuwa linafungwa na dili hilo limekuwa linachelewa kutokana na Dortmund kukataa kupunguza bei ya winga huyo.

Sancho mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na vigogo hao wa Bundesliga Agosti, 2017 akitokea Manchester City. Katika orodha ya wachezaji ambao Sancho aliwataja kuwa wana uwezo mkubwa wa kucheza mpira, alimtaja pia David Silva na Kevin de Bruyne miongoni mwa wachezaji watano bora aliowahi kucheza nao.

Alimtaja pia mchezaji mwenzake wa zamani wa Dortmund, Mario Gotze na winga wa sasa wa miamba hiyo, Julian Brandt.

“Nimewahi kucheza na Marcus Rashford na nimeona ana uwezo mkubwa, pia wakati nipo Man City nilicheza na Kevin de Bruyne na David Silva,” alisema.

Man United inataka kulipa Pauni 90 milioni kwa ajili ya kuinasa saini ya Sancho, lakini klabu yake ya Dortmund inahitaji Pauni 108 milioni ili kumuuza mchezaji huyo ambaye amecheza mechi 13 za timu ya Taifa ya England.

Advertisement

Ripoti zilizotoka wiki iliyopita zinadai Mkurugenzi wa Dortmund, Sebastian Kehl amesisitiza kwamba timu hiyo haina mpango wa kumuuza mchezaji huyo.

 

Advertisement