Solskjaer? bora Moyes

Muktasari:

Man United ilianza msimu kwa kasi, ikiichapa Chelsea 4-0 kwenye mchezo wa kwanza, lakini mechi iliyofuatia baada ya hapo ni sare dhidi ya Wolves, kisha iliyofuatia, ikachapwa na Crystal Palace. Si rekodi nzuri. Timu imeshinda, imetoa sare, imefungwa.

LONDON,ENGLAND .MANCHESTER United imeruka maji, imekanyaga moto. Unaambiwa hivi, Ole Gunnar Solskjaer ni mbovu kuliko makocha wengine wote, akiwamo David Moyes waliotua kuinoa Man United tangu Sir Alex Ferguson alipoondoka.

Wanasema hivi, namba hazidanganyi. Rekodi za ushindi wa Ole tangu alipotua Man United, mechi zake 32 za kwanza, ni mbovu kuliko Moyes, Louis van Gaal na hata Jose Mourinho, aliyembadili Desemba mwaka jana huko Old Trafford.

Ole ameshinda asilimia 53.1 tu ya mechi hizo 32, akilingana na Van Gaal wakati wenzake Mourinho ameshinda kwa asilimia 65.6 na Moyes asilimia 56.3. Kwa hesabu nyepesi tu, ni hivi Solskjaer amepoteza mechi 10 kati ya hizo 32 za kwanza alizoinoa Man United kwenye michuano tofauti. Jambo hilo linazua wasiwasi mkubwa.

Man United ilianza msimu kwa kasi, ikiichapa Chelsea 4-0 kwenye mchezo wa kwanza, lakini mechi iliyofuatia baada ya hapo ni sare dhidi ya Wolves, kisha iliyofuatia, ikachapwa na Crystal Palace. Si rekodi nzuri. Timu imeshinda, imetoa sare, imefungwa.

Kuondoa uwezekano wa kupotea kabisa, Man United inahitaji ushindi kwenye mchezo wake ujao, itakapokipiga na Southampton. Hii ni mechi ya lazima ushindi kwa Ole.

Kocha huyo raia wa Norway, tangu alipotua Man United amevuna pointi 56 na kwa kulinganisha na wenzake waliomtangulia walipocheza idadi kama hiyo ya mechi alizofikisha yeye kwa sasa, amezidiwa na wote, Moyes alivuna pointi 60 sawa na Van Gaal, wakati Mourinho alivuna pointi 69. Na mashabiki wa Man United wamevurugwa zaidi baada ya Chris Smalling kuruhusiwa kwenda kujiunga na AS Roma kwa mkopo na kuwabakiza kikosini Marcos Rojo na Phil Jones, ambao wao wiki uwanjani, wiki kwenye wodi ya wagonjwa.

Smalling alicheza mechi 34 kwenye michuano yote msimu uliopita na kitu kizuri kwake alifunga hata bao dhidi ya Watford. Rojo alicheza mechi sita tu na Jones mechi 24, huku Matteo Darmian akiwa mchezaji mwingine ambaye mashabiki wa timu hiyo wanamtaka aondoke.

Smalling anajiona wazi hayupo kwenye mpango wa Solskjaer kwa msimu huu na ndio maana ametafuta mahali ambako atapewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Kocha Ole, sasa kwa sasa anawaamini mabeki wa kati, Harry Maguire, Victor Lindelof, Eric Bailly na Axel Tuanzebe.