Siyo Bocco,Luis tu ... tutafunga busta kila mechi

Friday February 28 2020

simba vs Yanga,kocha wa simba,Sven Vandenbroeck,Yanga vs KMC,usajili wa wachezaji,KMC VS Azam,

 

By Mwandishi wetu

SIMBA imesisitiza haina presha hata chembe na mechi dhidi ya Yanga Machi 8 na wala haitampumzisha mchezaji yeyote kuelekea mechi hiyo.

Klabu hiyo pekee yenye Wabrazili wawili kwenye usajili wake, itacheza dhidi ya KMC na Azam kabla ya kuikabili Yanga, huku mashabiki wakionekana kuihofia zaidi mechi ya Azam.

Lakini benchi la ufundi limesisitiza kwamba mziki wao ni uleule tena wanaihofia zaidi KMC kuliko hata hao Yanga.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema; “Yaani tuhofie kuwachezesha wachezaji wetu eti kisa Yanga? Haitakuja kutokea.. kwani si ni timu kama nyingine tu. Yaani tuache kufikiri kupata pointi tatu dhidi ya KMC, Azam tuiwazie Yanga, yaani hilo wala haipo kabisa mawazoni mwetu kwa sasa.”

“Hivi hata ukisema uwapumzishe baadhi ya Wachezaji kwa kuhofia kadi au majeruhi ndio tutapata faida gani? Ninachojua hata mazoezini mchezaji anaweza kuumia na kadi unaweza kupata popote, hivyo kwa saa tunataka pointi tatu za KMC, Azam ndipo tutaanza maandalizi kwa ajili ya Yanga,”alisisitiza Patrick ambaye ni miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba.

Naye Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema mechi ya Jumapili dhidi ya KMC ndiyo inayomuumiza zaidi wala Yanga haimpi presha ana wachezaji wenye ubora wa kuwakabili kirahisi kama timu nyingine.

Advertisement

Ndani ya siku 10, Simba itacheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara, dhidi ya KMC Jumapili, kisha Machi 4 itaikabili Azam kabla ya kukwaana na maswahiba wao wa kitambo, Yanga wikiendi ya Machi 8.

Kutokana na homa ya pambano la hilo kupanda inadaiwa baadhi ya vigogo wamekuwa wakilishawishi benchi la ufundi kuwapunguzia muda wa kutumika baadhi ya mastaa ili kuwaanda kwa kipute hicho.

Katika mchezo uliopita wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Stand United, Kocha Sven aliwapumzisha washambuliaji wake John Bocco ‘Adebayor’ ,Luis Miquissone,Shomari Kapombe, Mohammed Hussein’Tshabalala’,Erasto Nyoni, na kipa Aishi Manula ambao walianza katika mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United.

Pia, kocha huyo licha ya kumuanzisha benchi beki Pascal Wawa katika mchezo dhidi ya Stand lakini hakumchezesha mpaka mechi ilipomalizika.

Advertisement