Sio Serengeti Boys tu unaambiwa

Thursday April 25 2019

 

By Charles Abel

SERENGETI Boys imetolewa kwa aibu kwenye mashindano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) huku ikiwa ndio timu iliyoruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi zaidi, ikiwa imefungwa mabao 12.

Wakati Watanzania wakishangazwa na rekodi hiyo isiyovutia, historia ya mashindano hayo inaonyesha kuwa pamoja na Serengeti Boys kuruhusu idadi kubwa ya mabao kwenye fainali hizo, bado haijavunja rekodi iliyowekwa na Shelisheli mwaka 2001, ya kuwa timu iliyoruhusu idadi kubwa ya mabao kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Timu hiyo ya taifa ya vijana ya Shelisheli wenye umri chini ya miaka 17 ilijikuta ikikung’utwa jumla ya mabao 17 kwenye fainali za AFCON U17 zilizofanyikia nchini kwao mwaka huo.

Shelisheli waliokuwa kundi A walianza kwa kupokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Cameroon katika mchezo wa ufunguzi na mechi iliyofuata walichapwa mabao 4-1 na Burkina Faso kabla ya kupokea kichapo kitakatifu cha mabao 8-0 kutoka kwa Mali na walimaliza wakiwa wamefunga bao moja tu.

Hata hivyo kinyume Shelisheli, hakuna nchi nyingine mwenyeji wa mashindano ya AFCON U17 ambayo iliruhusu mabao mengi kwenye hatua ya makundi kulinganisha na Serengeti Boys kwani kabla ya mashindano ya mwaka huu, Gabon iliyoandaa mwaka 2017 na Botswana iliyoandaa mwaka 1997 ndizo zilikuwa zimefungwa mabao 11 kila moja kwenye hatua ya makundi.

Wakati Serengeti Boys ikiingia kwenye historia mbaya ya kuwa kwenye tatu bora ya timu mwenyeji zilizoruhusu idadi kubwa ya mabao kwenye hatua ya makundi ya AFCON U17, Morocco, Algeria na Rwanda zenyewe zimeweka rekodi ya kuwa timu mwenyeji zilizofungwa mabao machache zaidi kwenye mashindano hayoa ambapo kila moja iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili pindi zilipoandaa mashindano hayo kwa nyakati tofauti.

Advertisement

Kocha msaidizi wa Serengeti Boys, Maalim Salehe aliliambia Mwanaspoti kuwa udhaifu wa safu ya ulinzi ndio sababu kuu ya kuifanya iruhusu idadi kubwa ya mabao.

“Hatukuwa tunacheza vibaya lakini kama ambavyo mmeona vijana wetu walifanya makosa ambayo yametuangusha.

Lakini tukumbuke kuwa hawa ni watoto, kwa hiyo jambo la msingi ni kuangalia tunawajenga vipi ili vipaji walivyonavyo viwe na msaada kwao na taifa siku za usoni na kupata vijana watakaosaidia zaidi,” alisema Salehe.

Advertisement