Simba yaizunguka Yanga SC kimafia!

HAPA ni mwendo wa kupindua meza tu, yule straika Mghana, Michael Sarpong ambaye Kocha wa Yanga, Luc Eymael amependekeza asajiliwe, amepigiwa simu na mabosi wa Simba.

Sarpong ambaye ni huru amezungumza na Mwanaspoti kutoka Rwanda akathibitisha na ana ofa ya Yanga na wameshazungumza mambo mengi lakini hana uhakika kama atatua Jangwani kwa vile Simba nao wamempa maneno mazuri.

Anasema Simba wamempigia simu akawaambia kile anachotaka na wao wakamwambia watamjibu ngoja wakafanyie kazi mapendekezo yake ambayo hatahivyo hakuyaweka wazi.

“Nilikuwa na mazungumzo na Yanga kweli, nafikiri mambo yanaenda sawa hakuna shida nasubiri kuona kipi kitatokea hapo mbele,” alisema Sarpong ambaye Rayon Sports ilisitisha mkataba wake hivi karibuni baada ya kutoa kauli iliyotafsiriwa kama amemdhalilisha Rais wa klabu hiyo anapwaya.

“Sijajua nitacheza wapi kwa kuwa naona Simba nao wamenifuata wanaonyesha nia kubwa tu ya kutaka kunisajili sasa naangalia wapi kutakuwa bora zaidi kwangu kucheza na kufanya kazi yangu inavyotakiwa,”alisema na kuongeza aliyempigia simu alimwambia anasimamia usajili wa Simba.

“Nafikiria kufanya maamuzi sahihi kwa maisha yangu ngoja tusubiri haya mambo ya ugonjwa wa Covid 19 yapungue tujue nitafanya uamuzi gani.

“Nilipenda kufanya kazi hapa Kigali lakini mambo yaliyotokea hapa sikuyafurahia lakini sasa nataka kwenda sehemu ambayo sitapata shida tena ya kutekeleza uwezo wangu ndio maana nataka kuamua kwa usahihi zaidi,” alisema huku akisisitiza anaweza kusaini popote kwa vile hakuna ambaye wameshamalizana nae moja kwa moja.

Kocha Eymael amelithibitishia Mwanaspoti mchezaji huyo ni mkali wa kutupia na amempendekeza akijua atakuwa msaada mkubwa kwake msimu ujao kama wakimaliza dili lake kwa wakati.

Rayon inadaiwa kusitisha mkataba wa mchezaji huyo kutokana na kauli yake aliyojibu baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwaandikia barua wachezaji na makocha kusitisha mishahara yao mpaka corona itakapomalizika kwavile hawana vyanzo vyovyote vya mapato. Ingawa yeye amesisitiza alisema anadai mshahara wa miezi mitatu na mkataba wake umesalia miezi mitano hivyo hajadhalilisha mtu.