Simba wataja sababu za kumtimua Aussems

Muktasari:

Kupitia taarifa ya Simba iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingiza Mbatha, ilieleza kwamba imevunja mkataba na kocha huyo kuanzia leo Jumamosi Novemba 30 2019.

BAADA ya Kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems kuwahi kujitangaza mwenyewe kwamba amechana na timu hiyo baada ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Afisa Mtendaji mkuu wa timu hiyo, Senzo Mazingisa, Uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi sababu za kuachana naye.

 

Kupitia taarifa ya Simba iliyotolewa na Senzo ilieleza kwamba imevunja mkataba na kocha huyo kuanzia leo Jumamosi, Novemba 30 mwaka huu.

 

"Bodi imefikia  uamuzi huo baada ya Aussems kushindwa kutekeleza majukumu kwa viwango na malengo ambayo klabu ilikubaliana naye kwenye mkataba wa ajira, ikiwa ni pamoja na timu ya Simba kushindwa kufika hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2019/20,".

 

Taarifa hiyo ilieleza kwamba pamoja na jitihada zote za dhati bodi kumpa ushirikiano kocha huyo, bado Aussems aliendelea kusimamia timu bila kujali malengo ya Simba licha ya kujenga time yenye ari ya mafaniko, nidhamu  na ushindani kwenye michuano  ya ndani na nje ya nchi.

 

"Maelezo yaliyotolewa na kocha kwenye kikao na kamati ya nidhamu iliyokaa Novemba 28, 2019, hayakuiridhisha  kamati hiyo dhidi ya tuhuma za kocha kuondoka kituo cha kazi bila ruhusa  ya Uongozi wa Klabu, ikizingatiwa kocha kukataa kuiambia kamati sehemu aliyokwenda na sababu za kwenda bila ruhusa,".

 

Senzo aliandika "Bodi inatambua na kuthamini mchango wa kocha huyo kwenye mafanikio waliyoyapata katika kipindi chake, hata hivyo Uongozi unaona ni wakati muafaka sasa kwa klabu kuwania mafaniko ya mashindano ya kimataifa,".

 

Kuhusu mchakato wa kocha mpya timu hiyo utaanza mara moja na sasa itakuwa chini ya kocha msaidizi, Denis Kitambi mpaka atakapopatikana Kocha Mkuu.