Simba wapata hati mpya, wamshtaki Kilomoni TFF

Tuesday July 16 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Sakata la Simba na mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini Hamis Kilomoni limechukua sura mpya baada ya uongozi wa klabu hiyo kutangaza kupata hati mpya ya mali za Simba huku ikieleza kumshtaki Kilomoni kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Simba wamekwenda mbali zaidi na kubainisha kwamba, Kilomoni si Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba tangu Oktoba, 2017.

Hata hivyo, Kilomoni amewagomea akisisitiza mtu mwenye mamlaka ya kutangaza kuondolewa katika nafasi hiyo ni kamati ya utendaji ya Simba iliyochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema Kilomoni si mdhamini tena wa Simba na wajumbe wa Bodi ya wadhamini ni Abdul Abbas, Adam Idi Mgoyi, Juma Kapuya na Ramesh Patel.

Alisema klabu hiyo imefunga mjadara wa Kilomoni huku akibainisha kwamba tayari uongozi wa klabu umepata hati nyingine za mali za Simba huku ikipanga kumpeleka Kilomoni kwenye kamati ya maadili ya TFF.

"Tulimfuata kumuomba hati, tangu tumemuomba anatuzungusha, mdhamini mwenzake, Ramesh Patel amekwenda kwake kumtaka arejeshe hati akasema hadi aitafute, tukatangaza katika gazeti la Serikali kwamba imepotea, hatukuwa na sababu ya kumsubiri yeye na tumeshapata hati nyingine," alisema Magori.

Advertisement

Alisema Kilomoni sasa akiongea kama mdhamini hiyo ni jambo jingine kwani Kilomoni si mdhamini tena wa Simba," alisema Magori.

Hata hivyo Kilomoni amesisitiza kutotishwa na mkakati huo huku akihoji huyo aliyetangaza yeye si mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini anazungumza kama nani?," alihoji Kilomoni.

Alisema utaridhia kutoka Baraza la Wadhamini kama tamko hilo litatolewa na Mkwabi na kamati yake tendaji kwani hao ndiyo waliochaguliwa na wanachama wa Simba na si mtu mwingine yoyote.

 

Advertisement