Simba vs Tanzania Prisons : Mechi kali yenye rekodi flani hivi

Thursday November 7 2019

 

By Waandishi wetu

ACHANA na matokeo ya mechi za jana Jumatano kwenye viwanja tofauti ukiwamo ule wa Mtibwa Sugar dhidi ya Mwadui uliopigwa Uwanja wa CCM Gairo, unaambiwa kazi ipo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati vinara Simba itakapowakaribisha Maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.

Ishu hapa wala sio kitu kingine, bali ni rekodi zilizopo kwa timu hizo msimu huu mbali na zile za kukutana kwao jijini Dar es Salaam, lakini pia makocha wa pande zote walivyotamba kabla ya kuvaana ndani ya dakika 90, Patrick Aussems akitarajiwa kukipangua kidogo kikosi chake kwa leo.

Simba inaikaribisha Prisons ikiwa kinara kwa kucheza mechi nane na kukusanya alama 21 ikiwa timu yenye alama nyingi na mabao mengi, huku ikiwa imeruhusu mabao machache kuliko timu zote, lakini wakizidiwa ujanja na Tanzania Prisons, kwani Maafande hao ndio pekee hajawafungwa. Prisons inayonolewa na Kocha Mohammed ‘Adolph’ Rishard, licha ya kushuka uwanjani mara tisa imekusanya pointi 15, ikiwa ndio pekee ambayo haijaonja kipigo mpaka sasa ikizifunika vigogo vyote ikiwamo Simba, Yanga na Azam FC.

Mbali na rekodi tamu Prisons, bado timu hiyo haijashinda kwenye mechi ya jijini Dar es Salaam dhidi ya Simba, kitu kinachoufanya mchezo wa leo kuwa wa aina yake kwani, Kocha Adolph ameipoteze rekodi hiyo ya uteja akidai wanazitaka pointi tatu.

Katika michezo tisa walizocheza tangu mwaka 2009, Prisons imefumuliwa mara zote na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 21 na yenyewe kufunga mabao matatu tu, hali inayowafanya mashabiki wa Simba kuanza kusherehekea ushindi kabla chama lao halijashuka Uhuru.

“Tuna rekodi mbaya dhidi ya Simba, jijini Dar es Salam. Sawa kuna historia, lakini mambo ya mpira huwezi kuyahukumu kwa historia. Tunasubiri kitakachotokoea ndani ya dakika 90 za kesho(leo). Yaani kila kitu kitakuwa kipya, hivyo watu wasubiri kuona kitatokea nini,” alisema Kocha Adolph.

Advertisement

Kipigo kikubwa ambacho Prisons imekipata kutoka kwa Simba ni cha mabao 5-0 katika mechi iliyopigwa Februari 28, 2015 kwenye Uwanja wa Taifa, hata hivyo rekodi ya kutopoteza mchezo mpaka sasa inawapa jeuri maafande hao.

Awali Simba na Prisons ndizo zilizok

uwa zimebaki kama timu ambazo zilizokuwa hazijui ladha ya vipigo, lakini Mwadui ilitibulia Sinza Oktoba 30 ilipoifunga bao 1-0 mjini Shinyanga.

Yanga ilikuwa kigogo wa kwanza kupoteza mbele ya Ruvu Shooting kabla ya Azam kufanyiziwa pia na Simba na Ruvu katika mechi mbili mfululizo.

Kocha Aussems, alisema rekodi ya wapinzani wao Prisons kwa msimu huu wala sio tatizo kwao wanapokutana nao katika mchezo wa leo.

“Wanatukabili katika mchezo huu wakiwa na rekodi nzuri, lakini kwetu wala sio tatizo tumejipanga kufanya vizuri dhidi yao,” alisema Aussems aliyefichua wamepata muda wa kuwafuatilia wapinzani wao hao kujua wanachezajie na wamejiandaa kupambana kusaka alama tatu.

Katika mchezo mchezo wa leo Simba inaweza kuwa na mabadiliko kidogo kwani kwenye mazoezi ya mwisho jana asubuhi, Kocha Aussems alimuingiza Jonas Mkude na kumchomoa Mzamiru Yasin, huku pia kwenye nafasi ya beki ya kushoto akimpanga Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuchukua nafasi ya Gadiel Michael.

Kulingana na mazoezi ya jana wachezaji walionekana kama wa kikosi cha kwanza walikuwa ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Tshabalala, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Mkude, Francis Kahata, Sharafeldin Shiboub, Meddie Kagere, Clatous Chama na Ibrahim Ajibu.

Kocha Aussems alisema kumtumia Mkude kucheza na wale anaowatumia kikosi cha kwanza kumetokana na kuwa kwake fiti kimwili.

Alisema wachezaji atakaowakosa leo ni nahodha John Bocco na Mbrazili, Wilker Da Silva ambao jana walikuwa wakikimbi pembeni sambamba na Miraji Athumani chini ya Kocha Adel Zrane.

Advertisement