Simba sasa yakwepa Vigogo

WAKATI presha ikiwa imepanda kwa mashabiki wa Simba baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu na timua timua ya makocha wake na maofisa kuanza, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) limewapa ahueni baada ya kuiepusha kukutana na miongoni mwa klabu nane vigogo wa soka la Afrika kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Vipigo vya bao 1-0 ilivyopata mbele ya Prisons na Ruvu Shooting huku wakionyesha kiwango duni, vimeonekana kuwapa wasiwasi mashabiki na wadau wa Simba wakihisi huenda timu yao ikafanya vibaya tena kwa aibu katika Ligi ya Mabingwa Afrika hasa kama itapangwa na timu tishio zinazotamba kwa uwekezaji wa ndani na nje ya uwanja barani Afrika.

Hata hivyo, Caf imefanya uamuzi ambao huenda ukaleta ahueni kwao baada ya kuamua timu 10 kupenya moja kwenda raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na hivyo, kuondoa uwezekano wa kukutana na Simba mwanzoni. Na hata kama zitakwenda kukutana kwenye hatua ya kwanza, Simba ikijikwaa inaweza kuangukia Kombe la Shirikisho.

Katika kundi hilo la timu 10 zilizopenya moja kwa moja, mashabiki wa Simba hapana shaka watakuwa na furaha kubwa kusikia zimo timu nane ambazo kwa nyakati tofauti zimekuwa zikitamba kwenye mashindano ya klabu Afrika ikiwemo kutwaa mataji huku pia zikiwa na uwekezaji mkubwa wa kifedha na vikosi imara.

Vigogo hao nane ambao Simba imenusurika kukutana nao mapema ni Al Ahly na Zamalek za Misri, Wydad Casablanca na Raja Casablanca za Morocco, TP Mazembe na AS Vita Club (DR Congo), Esperance (Tunisia) na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Al Ahly ndio inaonekana kuwa tishio zaidi katika mashindano hayo kwani, ina uzoefu wa kutosha na imetwaa taji hilo mara nyingi zaidi ikifanya hivyo mara nane na kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili.

TP Mazembe yenyewe imetwaa ubingwa mara tano kama ilivyo kwa Zamalek, Esperance (4), Raja Casablanca (3), Wydad Casablanca (2) huku AS Vita na Mamelodi zikitwaa mara moja moja kila timu.

Kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa na Caf, timu hizo nane zitafuzu moja kwa moja raundi ya kwanza sambamba na timu nyingine mbili, Horoya (Guinea) na Primeiro de Agosto ya Angola.

Kwa vigogo hivyo nane kupenya moja kwa moja, Simba angalau inaweza kutokutana na changamoto ngumu katika raundi ya awali kutokana na uwepo wa kundi kubwa la timu ambazo zinaonekana kuwa daraja moja kiuwezo au kiuzoefu na Simba ama zimeachwa mbali kidogo.

Hata hivyo, katika kundi la timu 44 ambazo zitacheza hatua ya awali ikiwemo Simba, zipo timu kadhaa ambazo zinaonekana zinaweza kuwapa changamoto wawakilishi hao wa Tanzania katika mashindano hayo.

Miongoni mwa timu hizo ni CR Belouizdad na MC Alger za Algeria, Kaizer Chief (Afrika Kusini), Al Merrikh na Al Hillal (Sudan), Petro de Luanda (Angola) na Enyimba (Nigeria).

Kocha namchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Adolph Rishard, alisema; “Simba wana kazi kubwa, wanapaswa wajishike vizuri sana kuelekea michuano hiyo mikubwa Afrika, ninachokiona kwa sasa ndani ya Simba kuna wachezaji ndiyo wanawategemea zaidi kuwapa matokeo mazuri.

“Mashindano yote ni magumu hivyo sasa wasijipotoshe kwa kauli yao ya kuwa na kikosi kipana wanakokwenda ni kugumu zaidi, wakijiandaa vizuri hata kama wangekutana na Waarabu wangefanya vizuri ila wasipojipanga hata watakaokutana nao watakutana na wakati mgumu,” alisema Rishard.

Winga wa zamani wa Simba, ambaye kwa sasa ni kocha wa Pamba, Ulimboka Mwakingwe alisema; “Mpira hauchezwi gizani, kila mtu anaona namna Simba wanavyocheza, mfumo anaotumia kocha wao sioni kama una shida maana ndio huo huo uliokuwa unampa matokeo mazuri, hivyo kupoteza mechi mbili asilaumiwe mtu hata timu kubwa Ulaya. Benchi la Ufundi ndilo likae chini kuona namna gani wafanye ili mechi zijazo zikiwemo za kimataifa wafanye vizuri, naamini hilo linawezekana.

“Simba wataanza kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali ambapo, hawatakutana na timu za kiarabu lakini kama wamejipanga vizuri hata kama wangekutana nao wangefanya vizuri na si kwa mwenendo huu wa kutupiana lawama.

“Nitashangaa sana viongozi wa Simba wakimfukuza kocha, mpira wa si soka la mtu mmoja pekee kuleta mafanikio, kocha anafundisha mazoezini na hawezi kuingia uwanjani wakati wa mechi kuelekeza namna ya kufunga, wachezaji pia wanapaswa kujiongeza wakiona maji yamezidi unga,” alisema Mwakingwe.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema; “Nimemwangalia Sven ufundishaji wake ni kocha anayeweza.
Akiona mechi ngumu anajaza viungo na ndivyo inavyopaswa lakini hawezi kufanya kila kitu ndani ya uwanja ambapo, linabaki kuwa jukumu la wachezaji kujiongeza pale ambapo wanaona mechi imekuwa ngumu na wanataka matokeo.

“Kama Sven atakuwepo Simba basi mechi za Caf watafanya vizuri kuliko kocha aliyepita ambaye alikuwa anapigwa bao tano ugenini ila kama wachezaji ama viongozi wa Simba watachukulia kikosi chao ni cha kufanya vizuri ligi ya ndani basi watarajie kimataifa watafanya vibaya.

“Ninachohisi kuna tatizo baina ya viongozi na kocha maana nazielewa vizuri hizi timu, zikimchoka kocha basi wanaanza kumtafutia sababu ili timu ifanye vibaya jambo ambalo si zuri kwenye soka, Simba inapaswa kuwa na utulivu sasa,” alisema.