Simba isifanye dharau mechi za makundi Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

Al Ahly, Vita na hata JSS sio timu nyepesi kama ilivyo kwa wao Simba, hivyo kitu muhimu ni kujiandaa vya kutosha na kuwaaminisha wachezaji kwamba mechi za kundi lao hazitakuwa nyepesi na badala yake wakaze misuli ili kuivusha robo fainali.

TANGU ifanyike droo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wawakilishi wa Tanzania, Simba iliangukia Kundi D kumekuwa na mijadala na maneno mengi kutoka kwa mashabiki wa soka nchini.

Mashabiki hao wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya Simba kupangwa kundi moja na vigogo Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na JS Saoura ya Algeria, wengi wakiamini wawakilishi hao wamepangwa kundi la kifo na wengine wakiona ni jepesi.

Hata baadhi ya viongozi, wachezaji wa Simba na Kocha Mkuu, Patrick Aussems wamekuwa wakitoa maoni yao juu ya kundi hilo na nafasi ya Simba katika kuvuka ili kucheza robo fainali.

Kocha Aussems akiwathibitishia Watanzania kuwa, Simba itavuka kwa vile ana uzoefu wa michuano ya Afrika hata kama amepangwa na Al Ahly, Vita na JSS, kwani hata Simba ni timu kubwa na yenye uzoefu wa mechi kama hizo.

Hatuna tatizo na msimamo wa Kocha Aussems kwa vile hakuna kocha aliye tayari kukiri timu yake imepangwa na timu ngumu, hivyo haiwezi kuwa na nafasi ya kusonga mbele. Kwanza atawavunja nguvu wachezaji wake na mashabiki, pia anaweza kuonekana kituko mbele ya wadau wa michezo.

Hata hivyo, kwa wadau wa soka tungependa kuikumbusha Simba, wasijenge fikra na imani ya moja kwa moja wapo kwenye kundi jepesi. Makundi yote ya msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika ni magumu likiwemo hilo lao, hivyo ni wajibu wa wawakilishi wa Tanzania kujipanga kukabiliana na wapinzani wao.

Kama Simba itaamini imepangwa na timu nyepesi inaweza kuwafanya wakadharau michezo yao na kujikuta wakiumia, kama walivyoumia Yanga walipojikuta msimu uliopita wa Kombe la Shirikisho kupangwa na timu za ukanda wa Afrika Mashariki na kuamini wangekuwa na kazi nyepesi.

Yanga walipangwa kundi D la michuano hiyo sambamba na Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda na USM Alger ya Algeria na wengi wa wadau wa klabu hiyo waliamini moja ya nafasi mbili za kucheza robo fainali ni yao nyuma ya Waalgeria.

Kilichotokea ni kwamba Yanga ilinyooshwa ovyo katika kundi hilo, Gor Mahia wakijipigia nje ndani, Rayon waligoma kufungwa ugenini na kuicharaza Yanga ikiwa kwao, huku USM Alger ikishinda nyumbani na kulala ugenini mbele ya Jangwani.

Yanga na tumaini lao lote waliishia kushinda mechi moja tu, kutoka sare moja na zilizobaki kupasuka na kuwatibuliwa kiu yao ya kutinga robo fainali.

Kwa kuchelea Simba nao yasiwakute ya watani zao, ndio maana tunaikumbusha isidharau wapinzani wa kundi lao, kwani kama wakiingia kwa mtazamo huo kuwa timu wanazocheza nao ni nyepesi yatawakuta ya Mashujaa waliowang’oa Kombe la FA.

Al Ahly, Vita na hata JSS sio timu nyepesi kama ilivyo kwa wao Simba, hivyo kitu muhimu ni kujiandaa vya kutosha na kuwaaminisha wachezaji kwamba mechi za kundi lao hazitakuwa nyepesi na badala yake wakaze misuli ili kuivusha robo fainali.

Kuwaaminisha wachezaji kwamba wapinzani wao sio wepesi itawasaidia kucheza na nidhamu na umakini mkubwa, kitu kinachoweza kuisaidia Simba kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao zote iwe nyumbani ama ugenini.

Katika soka hakuna kitu kibaya kama kumdharau mpinzani wako, timu nyingi kubwa zimekuwa zikiumizwa kwa kushuka uwanjani wakiwadharau wapinzani wao, jambo ambalo Simba inapaswa kuepuka mapema.

Tunaamini Simba kwa kikosi ilichonacho na aina ya mwalimu waliyenaye wakicheza mechi zao kwa nidhamu ya hali ya juu na kujituma uwanjani ni wazi Watanzania wajiandae tu kuona kwa mara ya kwanza timu yao ikivuka hatua hiyo.

Wawakilishi wa mataifa mengine, katika mechi kama hizi huwa makini zaidi na wakitumia kila aina ya mbinu ili kupata matokeo mazuri ya kuwavusha hatua hiyo kwa kujua kuwa, huko kuna mamilioni ya fedha kutoka kwa wadhamini wa CAF.

Fedha hizo hizo zimekuwa msaada kwa timu nyingi katika kujitengeneza kuwa klabu kubwa na tajiri, kitu ambacho hata Simba inapaswa kuweka akilini mwao, hatua hiyo sio nyepesi na lazima ikaze misuli ili ifuzu iandikishe rekodi, lakini pia ijitajirishe.

Soka la kisasa linahitaji fedha, Simba ikiitumia vyema nafasi iliyopata msimu huu ya kutinga makundi na kusonga mbele ni wazi itaongelea bahati ya fedha na pia kusaidia kujiongezea heshima katika soka la kimataifa. Kazi kwao Vijana wa Msimbazi!