Simba SC, Yanga vita tofauti leo

Muktasari:

Yanga imekuwa na wakati mgumu katika michezo yake dhidi ya Biashara mkoani Mara.

Dar es Salaam. Wakati Simba ikiwa na kibarua cha kupigania hatima yake kwenye mbio za ubingwa dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Yanga inakabiliwa na deni la kumaliza unyonge wa ugenini dhidi ya Biashara United, zitakapokutana Uwanja wa Karume, Mara.

Baada ya kupoteza ushindi katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Prisons na Ruvu Shooting, mchezo wa leo jioni dhidi ya Mwadui FC ni fursa muhimu kwa Simba kutuliza hali ya hewa na kuendelea kuweka hai matumaini yake ya kutwaa taji la Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo.

Ikiwa pointi sita nyuma ya Yanga, lakini pia kuachwa kwa tofauti ya zaidi ya pointi nane na vinara Azam, ambao jana walicheza dhidi ya JKT Tanzania, Simba inalazimika kupata ushindi leo kwani kama itatoka sare au kupoteza na wapinzani wake wakapata ushindi, itazidi kuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kutetea ubingwa kwani pengo la pointi dhidi ya Azam na Yanga litazidi na njia pekee ya kujinusuru na hilo ni kupata ushindi leo.

Katika kuzisaka pointi tatu, Simba pia ina kiu ya kurejesha makali yake ya kufumania nyavu baada ya kucheza mechi mbili bila kufunga bao ikichapwa kwa bao 1-0 katika kila mechi iliyocheza dhidi ya Prisons na Ruvu Shooting.

Bahati nzuri kwa Simba, ambayo leo bila shaka itamuanzisha nahodha wake, John Bocco katika nafasi ya ushambuliaji ni udhaifu wa safu ya ulinzi ya Mwadui FC, ambayo imetoka kupoteza kwa mabao 6-1 nyumbani dhidi ya JKT Tanzania.

Lakini pia inaweza kumtumia kiungo wake, Clatous Chama, ambaye amekosa michezo miwili iliyopita ambayo yote walipoteza jambo linaloweza kulipa ahueni benchi la ufundi la Simba katika mchezo wa leo.

Kocha wa Mwadui, Khalid Adam alisema matokeo yaliyopita wameyaondoa akilini na sasa wanaufikiria mchezo dhidi ya Simba pekee.

“Ni kweli tumefanya vibaya katika mchezo uliopita, lakini hii ni mechi nyingine na mbinu huwa tofauti, hivyo yaliyopita nyuma hatuyawazii kwa sasa na tunaangalia mechi dhidi ya Simba,” alisema Adam.

Mkoani Mara katika Uwanja wa Karume, Yanga itakaribishwa na Biashara United huku ikiwa na vibarua viwili vikubwa ndani ya dakika 90 za mechi hiyo.

Kibarua cha kwanza ni kusaka pointi tatu ambazo zitawafanya ama wakae kileleni mwa msimamo wa ligi au waendelee kuipa presha Azam FC, lakini cha pili ni kuvunja uteja ilionao dhidi ya Biashara United kila wanapokutana katika uwanja huo.

Biashara United, ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa msimu wa tatu sasa, haijawahi kupoteza mchezo wowote nyumbani dhidi ya Yanga na katika mechi mbili za misimu miwili iliyopita ambayo ilikuwa katika Uwanja wa Karume, imepata ushindi mara moja na kutoka sare moja.

Mara ya kwanza timu hizo kukutana katika Uwanja wa Karume, Musoma ilikuwa Mei 10, 2019, Biashara United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na mara ya pili ambayo zilitoka sare ya bila kufungana ilikuwa ni Julai 5 mwaka huu.

Hata hivyo, matokeo ya jumla ya mechi nne za Ligi Kuu zilizokutanisha timu hizo, yanaonyesha kuwa Yanga ni mbabe na wameibuka na ushindi mara mbili, Biashara wakishinda moja na nyingine wakitoka sare.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema timu yake inaingia kwa tahadhari kubwa katika mechi hiyo.

“Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri, hivyo unavyocheza nao unapaswa kucheza kwa umakini wa hali ya juu na kuepuka kufanya makosa, ambayo yanaweza kutugharimu, lakini pia kuhakikisha tunatumia vyema nafasi tutakazopata,” alisema Baraza.

Ukiondoa mechi hizo, leo pia kutakuwa na michezo mingine. Namungo watakuwa nyumbani kuialika Dodoma Jiji FC na mjini Sumbawanga, Prisons wataikaribisha Polisi Tanzania, ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, saa 8 mchana.