Simba:Deo Kanda Yanga? Thubutu!

Muktasari:

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa aliiambia Mwanaspoti jana kwamba: “Kanda ni mtu muhimu sana ndani ya Simba na bado tunamhitaji.” Lakini kiongozi mwingine mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba licha ya kugoma kutajwa jina lake, alisema: “Tunajua Yanga wanawapigia simu wachezaji wetu, lakini nataka nikuhakikishie kwamba hawawezi kusajili mchezaji yeyote Simba, hawana jeuri hiyo, wana vimeo vingi.”

KIKAO cha wiki mbili cha Yanga wamekubaliana kwamba piga ua lazima winga wa Simba, Deo Kanda wamalizane naye fasta na msimu ujao atue Jangwani.

Yanga wameshamseti mpaka muwezeshaji wao, GSM kwamba Kanda ni mmoja wa vichwa muhimu wanavyovitaka kwa msimu ujao.

Lakini Simba wamesikia kinachoendelea wakaguna na kudai Yanga hawana ubavu kwani wana vimeo vingi ambavyo haviwezi kuwafanya wamudu gharama za kumng’oa staa yeyote ndani ya Simba achilia mbali Kanda.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa aliiambia Mwanaspoti jana kwamba: “Kanda ni mtu muhimu sana ndani ya Simba na bado tunamhitaji.” Lakini kiongozi mwingine mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba licha ya kugoma kutajwa jina lake, alisema: “Tunajua Yanga wanawapigia simu wachezaji wetu, lakini nataka nikuhakikishie kwamba hawawezi kusajili mchezaji yeyote Simba, hawana jeuri hiyo, wana vimeo vingi.”

Kanda yuko Simba akimalizia mkopo wake wa mwaka mmoja akitokea TP Mazembe na Mwanaspoti linajua kwamba tayari amewaambia Simba wampe mkataba mpya kwani hafikirii kurudi Mazembe amelipenda bata la Msimbazi.

Meneja wa Kanda, Nestor Mutuale ameliambia Mwanaspoti kwamba mpaka sasa Yanga haijawasilisha ofa yoyote kwao, lakini endapo Simba wakimtaka au Yanga wanatakiwa kufuata njia sahihi.

Mutuale alisema amezungumza na Kanda ambaye bado yuko nchini akijificha akihofia ugonjwa wa Corona na kwamba bado winga huyo amemhakikishia ana furaha ya kubaki Simba hata kwa muda zaidi.

Bosi huyo alisema kuwa endapo Yanga inamtaka inachotakiwa ni kuwafuata Mazembe ambao ndio wenye mkataba wake kisha kumalizana nao kama ambavyo Simba ilifanya hapo kabla.

“Kanda hana tatizo Yanga wanatakiwa kuhakikisha kama wataweza kufikia kumlipa mshahara ambao Simba wanamlipa sasa ndipo wawafuate Mazembe waongee nao wataelewana,” alieleza Mutuale na kudai kwamba kiasi anacholipwa ni siri yake na mwajiri wake na Yanga wakienda wataambiwa.

“Kanda mpaka jana (juzi) naongea naye hajaongea na mtu yeyote wa Yanga lakini pia anapenda kubaki Simba hata kwa muda zaidi endapo watahitaji kufanya hivyo.

“Mkataba wake ukimalizika mwisho wa msimu huu Simba kama haitaki kuendelea naye basi atarudi Mazembe ambao wanaona kila kitu anachofanya Simba lakini najua Kanda hataki kurudi Congo sasa ameshafurahia maisha ya hapo Tanzania,” aliongeza Mutuale.