Simba, Yanga ziwe na heshima kwa Mtibwa, Ruvu na Coastal Union

Muktasari:

Na hii husababishwa na mambo kadhaa ambayo kama klabu inaweza kuyafanyia kazi na kuhakikisha hayatokei, inaweza kutamba na kutikisa kama ambavyo Leicester City walifanya katika Ligi Kuu ya England msimu wa 2015/2016.

KUNA ushindani wa hali ya juu katika Ligi Kuu Tanzania Bara kabla hata kila timu haijafikisha nusu ya idadi ya mechi zote 38 ambazo kila moja itacheza.

Na dalili za uwepo wa ushindani mkubwa msimu huu zimeanza kuonekana kutokana na aina ya matokeo ambayo timu zimekuwa zikiyapata katika michezo ambayo imekuwa ikiendelea.

Ukiondoa Prisons ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa, timu nyingine 19 zilizobakia zote zimeonja ladha ya kupoteza mechi hata zile tunazoziita ‘giant teams’ (klabu kubwa).

Katika hali ya kushangaza wakati ligi hiyo ikiwa katika raundi ya tisa, klabu za Yanga na Azam zime-shindwa kuingia hata katika kundi la timu 10 zilizo katika nafasi ya juu ndani ya msimamo wa ligi hiyo ingawa zenyewe zimecheza idadi ndogo ya mechi kulinganisha na nyinginezo.

Hata hivyo, bado huo hauwezi kuwa utetezi kwani Azam iwapo ingepata ushindi katika mechi zake zote tano ilizocheza hadi sasa, leo hii huenda ingekuwa nafasi ya tatu kama ilivyo kwa Yanga ambayo laiti ingepata ushindi katika michezo yake yote minne iliyocheza walau ingekuwepo nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.

Kuna dhana imejengeka kwamba hizo timu zinazoonekana ndogo huwa zinakuwa na nguvu ya soda kwani nyakati kadhaa hufanya vizuri mwanzoni na kisha baadaye zinaporomoka na kuzipisha zile kubwa.

Lakini hili halina uhalisia kwa sababu ligi huwa na ‘formula’ na kanuni zake, na kila timu inapoingia kwenye ligi inakuwa na lengo la kutwaa ubingwa.

Kutokana na aina ya matokeo ambayo inayapata kadri msimu unavyozidi kusogea ndipo malengo huanza kubadilika na baadhi ya timu hujikuta zinapigania kubaki Ligi Kuu.

Na hii husababishwa na mambo kadhaa ambayo kama klabu inaweza kuyafanyia kazi na kuhakikisha hayatokei, inaweza kutamba na kutikisa kama ambavyo Leicester City walifanya katika Ligi Kuu ya England msimu wa 2015/2016.

Moja ya sababu hizo ni ‘Fatigue’ ambao tunaita kwa lugha ya Kiswahili, uchovu. Huu hupo wa aina mbili ambazo ni ‘Mental Fatigue’ na ‘Physical au Muscles Fatigue’.

‘Mental Fatigue’ ni uchovu wa kiakili ambao huu unakuwa una athari ya kisaikolojia zaidi wakati Physical Fatigue ni ule wa kimwili.

Lakini pia wakati mwingine ni kutokana na sababu za kiuchumi na majeruhi ambazo hupunguza ufanisi wa kitimu na wachezaji kiujumla.

Kinachoonekana sasa kwa timu nyingi kufanya vizuri ni kitu kinachoitwa ‘Endurance’. Wachezaji wako imara na ‘fresh’ kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kabla ya msimu kuanza.

Lolote linaweza kutokea na hizo timu zikatikisa lakini kuna jambo lazima lifanye nalo ni kuhakikisha zinatumia mbinu zao zote na pia wachezaji kujitolea.

Kwa upande wa timu ambazo soka lake limenikosha hadi sasa ukiachana na hizo kubwa, naweza kuzitaja Namungo, Polisi Tanzania, Alliance, Prisons na hata Ruvu Shooting.

Kwanza zina muunganiko mzuri wa kitimu, wachezaji wake wanajituma lakini pia zinacheza kwa nidhamu ya hali ya juu kulinganisha na timu nyingine.

Kama zitaweza kuendelea na kasi ambayo zimeanza nazo, naamini zitafanya vizuri zaidi ya hiki ambacho zinafanya.