Simba, Yanga zakwepa jua, hawa wengine litawahusu

LIGI Kuu Bara inaendelea baada ya kuanza Septemba 6, huku asilimia kubwa ya timu 18 za ligi hiyo zimeshacheza mechi za raundi ya pili kila mmoja.

Hata hivyo wakati ligi ikiendelea Mwanaspoti limebaini kuna timu zitapata shida sana ya kucheza juani msimu huu hasa timu za maafande.

Uchunguzi uliofanywa kupitia ratiba ya ligi hiyo umebaini kuwa mzunguko wa kwanza pekee kuna timu 10 zitakuwa na kibarua kizito cha kutafuta pointi tatu wakati wa jua kali zikiwa na mechi kuanzia tano mpaka nane.

Timu kongwe Simba na Yanga zote hazina mechi hata moja ya mchana, huku Azam ikiwa na mechi mbili za saa 8 mchana dhidi ya Mbeya City Septemba 20 na Ihefu Oktoba 17

Hata hivyo timu za majeshi ndio zimeonekana kuathirika zaidi na ratiba ya kucheza juani kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi msimu huu.

Timu kama JKT Tanzania, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting ndizo zimeonekana zitacheza mechi nyingi mchana kwenye mzunguko huo wa kwanza wa ligi kuliko timu nyingine yoyote.

JKT Tanzania imepangwa kucheza mechi nane mchana na tayari imeshacheza mechi moja Jumamosi na kukubali kipigo cha bao 2-0 kutoka kwa timu iliyopanda daraja ya Dodoma Jiji FC.

Pia Septemba 18 itacheza mechi nyingine ya mchana dhidi ya maafande wa Polisi Tanzania, wakati Oktoba 10 itacheza saa 9:00 mchana na Ruvu Shooting.

Ratiba inaonyesha Oktoba 19 itacheza saa 8:00 mchana dhidi ya Prisons, Novemba 13 itaikabili Mbeya City saa 9:00 mchana, Novemba 21 itacheza na Gwambina saa 9:00 mchana, Desemba 12 itaikabili Biashara Unites saa 9:00 mchana wakati Desemba 28 itaumana na KMC saa 8:00 mchana.

TIMU NYINGINE

Timu nyingine yenye mechi nyingi za mchana ni Prisons ambayo ina mechi nane na itaanza dhidi ya Namungo Septemba 18, kisha Oktoba 19 itaikabili JKT Tanzania na itaumana na maafande wenzao Polisi Tanzania saa 9:00 mchana Oktoba 31.

Pia itaonyeshana kazi na Ruvu Shooting Novemba 14 kabla ya Novemba 22 kupambana na Mtibwa Sugar saa 9:00 mchana, Novemba 29 itaumana na Mwadui saa 8:00 mchana kama itakavyopambana na Coastal Union Desemba 13 na Gwambina Desemba 19 kwa muda huo.

Pia timu nyingine itakayopata tabu kucheza juani kwenye mzunguko wa kwanza ni Ruvu Shooting ilianza jana Jumapili kuikabili Ihefu kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya saa 8:00 mchana, pia itacheza na Biashara United Septemba 27, kisha itavaana na ndugu zao JKT Tanzania Oktoba 10 saa 9:00 mchana.

Ruvu Shooting itaendelea kupigia juani kwa kupambana na KMC katika mchezo utakaofanyika saa 8:00 mchana Oktoba 17, kisha itaikabili Coastal Union Novemba Mosi saa 9:00 mchana, itaumana na Prisons saa 8:00 mchana Novemba 14 halafu itamaliza na Namungo Desemba 26.

MBEYA CITY IMO

Timu nyingine ambazo zitapata dhahama ya kucheza juani ni Mbeya City ambayo ina mechi tano kwenye mzunguko wa kwanza na tayari moja ilishacheza kwenye ufunguzi wa ligi Septemba 6 ilipokubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa KMC katika mchezo uliofanyika saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dra es Salaam.

Pia timu hiyo inakabiliwa na mechi za mchana dhidi ya Azam(Septemba 20), Dodoma Jiji (Oktoba 11), JKT Tanzania Novemba 13 na Mtibwa Sugar Novemba 28.

KMC nayo ina mechi tano za mchana dhidi ya Mbeya City(Septemba 6 ilishinda mabao 4-0), Mwadui (Septemba 21), Kagera Sugar (Septemba 25) Ruvu Shooting (Oktoba 17) na JKT Tanzania Desemba 27.

Gwambina ina mechi za mchana dhidi ya Ihefu Oktoba 3, JKT Tanzania Novemba 21, Dodoma Jiji Desemba 13, Prisons Desemba 19 na Mbeya City Desemba 28 wakati Namungo ina mechi tano za mchana dhidi ya Coastal Union Septemba 6 iliposhinda bao 1-0, Prisons (Septemba 18), Ihefu (Oktoba 24),Biashara United (Desemba 5) na Ruvu Shooting Desemba 26.

Mtibwa Sugar pia ina mechi tano za mchana dhidi ya Biashara United (Oktoba 4),Kagera Sugar (Novemba Mosi), Coastal Union (Novemba 7), Prisons (Novemba 22) na Mbeya City (Novemba 28) wakati Ihefu ina mechi tano za saa 8:00 mchana dhidi ya Ruvu Shooting (Septemba 13), Gwambina (Oktoba 3), Azam (Oktoba 17), Namungo (Oktoba 24) na Polisi Tanzania (Oktoba 21).

Timu nyingine yenye mechi tano za mchana ni Biashara United ambayo itakuwa na kibarua cha kupambana na Ruvu Shooting Septemba 27, Mtibwa Sugar (Oktoba 4), Polisi Tanzania (Oktoba 25), Namungo (Desemba 5) na JKT Tanzania Desemba 12.

Dodoma Jiji Fc, Polisi Tanzania na Coatsal Union zina mechi nne nne za mchana wakati Mwadui ina mechi tatu na Azam ina mechi mbili.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa anasema ilitakiwa kila timu ionje joto la kucheza mchana na isiwe kwa baadhi ya timu tu.

“Sio haki kwamba baadhi ya timu ndio ziwe na mechi nyingi wakati wa jua kali na nyingine hazina kabisa. Hata Ulaya timu kubwa kama Chelsea, Manchester United kuna wakati unaona zinacheza mchana kwa nini hapa ishindikane.

“Wawe wanaangalia na hizo ratiba wanavyopanga sio baadhi ya timu zinacheza mechi zote jioni au usiku tu wakati nyingine zinaumia juani,hata kiafya sio nzuri kwa wachezaji”, anasema Mkwasa.

Naye kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed’ Bares’ anasema kucheza mchana ni kazi sana lakini hawana jinsi kwani ratiba ndio imeshapangwa.

“Sijui kitu gani kimekusudiwa mpaka timu zetu hasa hizi za jeshi kuwa na mechi nyingi mchana lakini acha tucheze,” alisema Bares.