Simba? Shida ni Ajibu, Ndemla

Saturday October 24 2020
ajibu pic

WAKATI ile kauli ya Simba kuwa ina kikosi kipana ikionekana kuacha maswali baada ya kipigo cha bao 1-0 juzi dhidi ya Tanzania Prisons, nyota wa zamani wa Simba wamekiangalia na kueleza kuwa kocha Sven Ludwig afanye kitu kabla ya mashindano ya kimataifa.

Lakini baadhi yao wameweka wazi kwamba wazawa Ibrahim Ajibu na Said walikuwa sehemu ya tatizo kwenye mchezo huo.

Simba juzi ilicheza ugenini bila wachezaji wake sita kina Clatous Chama, Meddie Kagere, Chris Mugalu, Serge Wawa, Gérson Fraga na John Bocco. Bocco na Kagere waliachwa Dar es Salaam kutokana na majeraha, Mugalu aliumia dakika za mwisho kabla ya mechi, Chama na Wawa wameenda kwao huku Fraga ni mgonjwa.

“Maana ya kikosi kipana ni kwamba una timu mbili ambazo zinaweza kucheza mechi kwa wakati mmoja na kukupa matokeo, ila kwa mazingira ya mechi ya juzi bado Simba inapwaya,” alisema kipa wa zamani Mosses Mkandawile.

Alitolea mfano kukosekana kwa Chama, nafasi yake ingezibwa na Ibrahim Ajibu, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Yanga ameshindwa kubadilika kiuchezaji.

“Ajibu ni mchezaji mzuri sana ni levo za kina Chama, tatizo lake yuko sloo sana akibadilika na kuwa na kasi kama alivyo Chama, Simba tungemsahau kitambo Mzambia huyo,” alisema.

Advertisement

Emmanuel Gabriel ameshauri kocha kuwapa nafasi japo kwa dakika chache wachezaji wote ili kuendana na ile dhana ya kwamba Simba ina kikosi kipana. “Kutopewa nafasi kwa Said Ndemla, Ibrahimu Ajibu na wengineo hakumaanishi hawana uwezo, ila wanakosa uzoefu, hilo linaweza kuwagharimu hata kwenye mechi za kimataifa kama ikitokea wanaocheza mara kwa mara wameumia,” alisema.

Gabriel alisema kipigo hicho kimethibitisha Simba ni moto ikiwa na washambuliaji, kinyume na hilo inakuwa na changamoto ya kuzuia mashambulizi na ina tatizo la kufungwa mabao ya krosi, hivyo kocha alifanyie kazi.

Mbali na nyota hao, kocha Abdul Mingange wa Lipuli alitaja mambo mawili yanayoisumbua Simba ambayo ni aina ya uchezaji na pia anafikiri Sven ni kama hawaamini baadhi ya wachezaji. “Simba ilikosa mpango mbadala katika mechi hiyo ambayo Prisons iliwazibia njia ikawa ngumu kupenya ngome, kingine nilichokibaini kocha ni kama hawaamini baadhi ya wachezaji, hivyo hawapi nafasi, wanakosa uzoefu,” alisema.

Katika mechi hiyo, kocha aliwaanzisha Hassan Dilunga na Charles Ilanfya, baadaye aliwaingiza Miraji Athuman na Kennedy Juma ambao kwa sasa hawana nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza alisema Simba inapaswa kurekebisha eneo la ulinzi ili izibe mianya ya kuruhusu mabao mepesi katika majukumu mazito yaliyopo mbele yao.

“Kama wamesajili kikosi kipana kinatakiwa kiwe msaada kwenye nyakati ambazo wengine wanapata shida,” alisema.

Advertisement