Simba, Prisons, Singida zaweka rekodi

Muktasari:

Timu iliyofunga mabao machache zaidi msimu huu ni Singida United yenye mabao 23 huku pia ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi 73.

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara Simba, Prisons na Singida United zimeweka rekodi tofauti kwenye msimu wa ligi 2019/20 uliomalizika jana Jumapili.

Ligi hiyo imekuwa mbaya kwa Ndanda yenye pointi 41, Lipuli (44) na Alliance(45) ambazo zimeungana na Singida United kushuka daraja moja kwa moja huku Mbao yenye pointi (45) na Mbeya City(45) zikipata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano na kama zitapoteza nazo zitashuka daraja na zikishinda zitaendelea kusalia kwenye ligi msimu ujao.

Simba imekuwa timu pekee iliyoshinda mechi nyingi kwenye ligi hiyo ikiwa imeshinda michezo 27 ikifuatiwa na Azam iliyoshinda 20 wakati Yanga ni ya tatu kwa kushinda michezo 19.

Wakati Simba ikiwa kinara wa kushinda mechi nyingi, Singida United ambayo tayari nimeshuka daraja imekuwa ndio timu pekee iliyoshinda michezo michache na kupoteza mingi msimu huu.

Timu hiyo imeshinda michezo minne tu katika mechi 38 ilizocheza msimu huu huku ikipoteza michezo 28, ikifuatiwa na KMC na Lipuli ambazo zilipoteza michezo 18 kila mmoja.

Maafande wa Prison wao wameweka rekodi ya kuwa timu iliyopata sare nyingi msimu huu, ikiwa imetoka sare michezo 19 ikifuatiwa na Yanga na JKT Tanzania ziliyopata sare michezo 15 kila moja huku Biashara United na Ndanda zikivuna sare 14 kila mmoja.

Kwa upande wa kuzifumania nyavu, Simba imeongoza kwa kufunga mabao mengi msimu huu ikifunga mabao 78 ikifuatiwa na  Azam iliyofunga mabao 52 wakati Namungo ni ya tatu ikiwa imefunga mabao 46.

Kocha wa Prisons, Mohammed Adolph Rishard amekiri kuwa sababu kubwa iliyosababisha kupata sare nyingi msimu huu ni ubutu wa safu yake ya ushambuliaji hivyo kuahidi kuiongezea nguvu msimu ujao kaa ataendelea na kikosi hicho.

 

"Kweli tulikuwa na shida kubwa katika safu ya ushambuliaji kwani licha ya kwamba tulikuwa tunatengeneza nafasi nyingi lakini tulishindwa kufunga mabao jambo lililosababisha mara nyingi kumaliza michezo yetu na sare nyingi"

 

"Msimu ujao Mungu akipenda tutahakikisha tunaongeza nguvu eneo la ushambuliaji  kwani mpira magoli," amesema Rishard.