Simba, Al Ahly lazima kieleweke

Tuesday February 12 2019

 

By Khatimu Naheka na Thobias Sebastian

MECHI ya kisasi, ndivyo unavyoweza kusema wakati Simba leo Jumanne itakapokuwa na kazi moja tu ya kuwamaliza Waarabu wanaocheza nao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika na wawakilishi hao wa Watanzania watakuwa na kazi moja tu ya kulipa kisasi cha kipigo cha aibu nahodha wao Msaidizi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amefunguka mazito juu ya walichopanga katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka.

Simba inakutana na Al Ahly ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupokea kipigo cha mabao 5-0 kule Borg de Arab jijini Alexandria, Misri.

Kumbuka pia kabla ya mchezo huo Wekundu hao walipigwa tena kwa idadi kama hiyo jijini Kinshasa dhidi ya wenyeji AS Vita Club.

Wakati Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems akitarajiwa kupangua kikosi chake na kile kilichocheza ugenini, nahodha msaidizi wa timu hiyo, Tshabalala ametoa tamko kuwa Ahly walishinda kwao na leo ni zamu yao nao kushinda Uwanja wa Taifa.

Tshabalala alisema kila kitu kwao kimekamilika na mbinu walizopewa na kocha wao, Patrick Aussems basi hata kwao bao 1-0 Ahly litawatosha muhimu ni pointi tatu.

“Tulichojifunza kama wachezaji ni kwamba mechi hizi za makundi Caf kila timu inataka kushinda nyumbani, nikweli tulipoteza vibaya ugenini ila kesho (leo) tuko nyumbani tunataka kushinda,” alisema Tshabalala.

“Tunahitaji kufufua matumaini ya kusonga mbele ni lazima tushinde mechi hii tunawaheshimu Al Ahly lakini tunataka ushindi wa hata bao moja au mengi muhimu zaidi ni pointi tatu.”

MAZOEZI YA MWISHO

Jana mchana Simba ilifanya mazoezi ya mwisho na Aussems alionekana kufikiria kufanya mabadiliko flani ya kikosi chake.

Akionyesha msisitizo wa kila mchezaji kitambua umuhimu wa kiheshimu nidhamu ya mchezo kocha huyo alikuwa mkali kuwapanga vijana wake ili wafanye kweli leo.

Aussems alianza kuwapanga Zana Coulibaly, Asante Kwasi, Pascal Wawa na Juuko Murshid kuwa katika ulinzi.

Kiungo akiwapa majukumu James Kotei, Jonas Mkude, Clatous Chama na Emmanuel Okwi huku pale mbele wakiwa nahodha mkuu, John Bocco na Meddie Kagere.

Kikosi hicho kilianza kuwapa presha wanachama wa Simba ambao walikuwa wakishuhudia mazoezi hayo wakiona kama kupangwa kwa Coulibaly na Kwasi kutawaumiza katika mechi hiyo na kuanza kununa na kuondoka uwanjani hapo wakienda nje kuweka vigenge vya kushauriana.

Hata hivyo, Aussems ni kama aliwasikia kisha kupangua nafasi hizo mbili akimrudisha Nicholas Gyan kulia na Tshabalala kushoto na jamaa wakasema hapo sawa.

Kocha Aussems alionekana wazi leo ataanza na mfumo wa 4-4-2 akitaka kuona timu unatafuta ushindi lakini pia ikiwa na nidhamu bora ya kuzuia na kupandisha mashambulizi.

OKWI KAGERE KAZI MAALUMU

Mganda Emmanuel Okwi katika mazoezi hayo alionekana kupewa jukumu maalumu la kupiga mipira yote ya adhabu ndogo akiwa katika uso wa lango.

Akipewa jukumu hilo Okwi alikuwa sambamba na Kagere na Bocco kuhakikisha wanashirikiana vyema katika jukumu hilo.

Kocha Aussems alimwekea vifaa maalumu Okwi vinavyotumika katika kupanga ukuta mithili ya watu kisha kumtaka kuwa ushirikiano na wenzake hao wawili katika kutumia nafasi hizo endapo zitatokea uwanjani.

Hata hivyo, baadaye Kocha Aussems aliwaongeza Chama na Mkude katika majukumu hayo ambao nao waliandaliwa sawasawa kuweza kufanikisha mbinu za ushindi.

WAARABU HAWA HAPA

Al Ahly ambao tayari iko nchini tangu juzi Jumapili baada ya kufanya mazoezi ya kwanza siku hiyo jioni pale Gymkhana jana jioni walitua katika uwanja wa mchezo.

Timu hiyo kupitia kwa kocha wao mkuu, Martin Lasatre raia wa Uruguay alisema hawakuja kutafuta sare bali ni kuchukua pointi tatu ili watinge hatua ya robo fainali.

Lasatre alisema hata kama waliifunga Simba 5-0 nyumbani kwao hiyo ni historia na sasa wanataka ushindi ugenini kama watapata nafasi hiyo.

“Tuliifunga Simba kwetu hiyo ni historia kwa kuwa mechi hiyo imeshapita sasa tunakuja katika mechi mpya na tofauti,” alisema Lasatre.

Beki huyo wa zamani wa Real Soceadad ya Hispania alisema Simba inaamini itakuja tofauti lakini kama watafanya makosa watayatumia kupata ushindi katika mchezo huo.

“Tunawaheshimu Simba wako nyumbani kwao tuliwafunga kutokana na kufanya makosa katika mechi iliyopita yakitokea tena makosa kama yale tutayatumia kuweza kupata ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kusonge mbele.”

Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kucheza leo Jumanne huenda kikawa hivi;

Aishi, Gyan, Tshabalala, Wawa, Juuko, Kotei, Okwi, Mkude, Kagere, Bocco na Chama.

Advertisement