Shirima kinda la Tanzania linalokimbiza Ukraine

KWA wale mashabiki wa muziki wa dansi bila ya shaka wanaukumbuka kile kibao cha Narudi Nyumbani, kilichomtangaza sana Dk Remmy Ongalla enzi za uhai wake, ambapo ndani kuna mstari unasema ‘Nyumbani ni nyumbani hata kukiwa kubaya au kuzuri...kwa baba yako ndiko kwako...’.

Dk Remmy aliimba akiwa na Super Matimila iliyokuwa inaundwa na wanamuziki mahiri na kutikisa nchini na duniani kwa ujumla.

Nimekitumia kipande hicho kutokana na kauli ya mchezaji chipukizi, Brian Shirima anayekiopiga Ukraine, nchi aliozaliwa ambaye anaseme licha ya kuzaliwa Ulaya hajasahau asili yake na kutaka siku moja kuchezea timu ya Taifa ya chini ya miaka 17, Serengeti Boys.

Brian, ambaye kwa sasa anacheza nafasi ya kipa katika timu ya Obolon Smena inayoshiriki katika Ligi Daraja la Kwanza, Baba yake, Rustice Shirima ni Mtanzania anayeishi na kufanya kazi nchini Ukraine. Mama yake ni Larysa Shirima, raia wa Ukraine.

Mchezaji huyo mwenye miaka 13, mpaka sasa amejipatia sifa kubwa katika mashindano ya vijana nchini humo na kuwa chagua la kwanza katika nafasi ya mlinda mlango katika timu yake.

Mpaka sasa Brian amefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya vijana mara tatu kuanzia mwaka 2017, 2018 na mwaka jana. Mashindano hayo yanaitwa ‘Ukrainian Children Championships.

Mbali ya mataji hayo, kipa huyo amefanikiwa pia kutwaa ubingwa wa mashindano ya Mji wa Kiev yajulikanayo kwa jina la Champions of Kiev and Kiev Region kwa miaka ya 2018 na 2019 na vilevile ameiwezesha klabu yake kutwaa ubingwa wa mashindano ya dunia ya World Trophy in Klagenfurt Austria (World Mini Trophy) mwaka 2017 na vile bile mashindano ya Ulaya ‘European Trophy in Sofia Bulgaria (Europe Mini Trophy) ya mwaka 2019.

Kama haitoshi, kinda huyo wa Tanzania ameweza kuisaidia timu yake kushinda taji la ligi ya kiangazi ya Ukraine ‘Ukrainian Summer Cup 2018/19 – Lutsk’ na kikubwa zaidi, aliiongoza timu yake akiwa nahodha.

Pia kama nahodha, aliiongoza vizuri timu yake kutwaa ubingwa wa kimataifa wa mashindano ya majira ya joto (kiangazi) ‘International Summer Cup 2019/20 na kikubwa katika kipaji chake, aliweza kuokoa penati tatu katika mechi ya fainali.

Mafanikio Binafsi

Pamoja na kuwa na umri mdogo, Brian alishinda nafasi ya pili ya kipa bora katika mashindano ya dunia kwa vijana ‘World Mini Trophy yaliyofanyika Klagenfurt, Austria na baadaye kushinda tuzo ya kipa bora katika mashindano ya bara la Ulaya ‘European Trophy’ yaliyofanyika jijini Sofia, Bulgaria.

Pia, alifanikiwa kushinda tuzo ya kipa bora katika mashindano ya majira ya joto (2019/2019 International Summer Cup Vinnitsa ambapo, alikuwa nahodha wa timu.

Timu ya Taifa ya Tanzania

Brian alisema kuwa pamoja na kuzaliwa Ukraine, kamwe hawezi kusahau asili yake na ndoto yake kubwa ni kuchezea timu ya Taifa ya Tanzania. Alisema kuwa anajivunia asili ya Tanzania na ameweka nadhiri kuwa siku moja atavaa jezi ya Taifa lake akiwakilisha katika mashindano ya kimataifa.

“Kaka yangu Christian amekwisha timiza ndoto yake katika mchezo wa kuogelea baada ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya Vijana yaliyofanyika mjini Budapest, Hungary mwaka jana kuanzia Agosti 28 hadi Septemba Mosi.

Kwa kweli amenitia moyo sana kuwa inawezekana, ila yeye kabla ya hapo alishiriki katika mashindano ya Taifa ya kuogelea akichezea klabu ya Dar Swim Club (DSC), mimi sina klabu, nategemea kuitwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),” alisema Brian. Alisema kuwa anaamini kuwa ndoto yake itafanikiwa na kuwa mmoja wa mashujaa katika soka na kuingia katika historia.

“Naamini, TFF haifahamu kuwa kuna Watanzania wanacheza soka Ukraine, ila kwa taarifa hii, najua sasa wataanza kutufuatilia kama Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA) kilivyomfuatilia kaka na kumchagua kwenye timu ya Taifa na kuiwakilisha nchi,” alisema.

Alisema kuwa wazazi wake wanampa sapoti kubwa sana kwani wanapenda waone vipaji vyao vinaendelea.

“Ukiondoa Christian, kaka yangu mkubwa, Adrian (19) amechezea klabu za Verona FC, Arsenal FC na Obolon FC pamoja na sasa kuwa majeruhi wakati ndugu yangu mwingine Antony – Jaysson naye anachezea klabu ya Obolon FC katika nafasi ya ulinzi, wote tupo vizuri na tunacheza kikosi cha kwanza,” alisema.

Historia yake

Brian, ambaye kwa sasa anasoma shule ya kimataifa ya Meridian mjini Kiev, alianza kucheza mpira akiwa na miaka saba (7) katika klabu ya daraja la kwanza ya Arsenal mwaka 2014 na mwaka 2015 alifanikiwa kuiwezesha klabu hiyo kushika nafasi ya pili katika mashindano ya ligi ya yoso ‘Ukrainian Children Championships’.