Shikalo : Nyie tulieni, mbona Yanga mtaipenda tu

Muktasari:

Kauli yake ilikuwa uthibitisho tosha kwamba vuta nikuvute iliyokuwepo kati ya Bandari na Yanga ambayo imekuwa ikimfukuzia tangu msimu uliopita, imefikia kikomo.

BAADA ya kutamba sana kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL), hatimaye kipa Farouk Shikalo amekamilisha uhamisho wake kutoka Klabu ya Bandari FC kujiunga na Yanga SC atakakokipiga kuanzia msimu ujao.

Shikalo ambaye pia ni kipa wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars, alithibitisha hivi majuzi kukamilika kwa makubaliano yote na Yanga, na vilevile kati ya klabu yake mpya na ile ya zamani Bandari FC ili kumruhusu aondoke.

Shikalo alithibitisha Jumamosi kwa kuposti kwenye akaunti yake ya Facebook kwamba anaondoka baada ya kuichezea Bandari katika michuano ya Cecafa inayoendelea nchini Rwanda ambako tayari wameondolewa. “Imekuwa ni misimu miwili ya kufana yenye mafanikio kibao na mafunzo. Ninachotaka kusema ni asante kwa benchi nzima la Bandari, wachezaji na mashabiki kwa sapoti kubwa waliyonipa kwa kipindi chote ambacho nimekuwa na klabu. Nawatakieni kila la heri katika siku za usoni,” aliandika Shikalo.

Kauli yake ilikuwa uthibitisho tosha kwamba vuta nikuvute iliyokuwepo kati ya Bandari na Yanga ambayo imekuwa ikimfukuzia tangu msimu uliopita, imefikia kikomo.

SAFARI YAKE

Hadi misimu miwili iliyopita hakuna aliyekuwa akilifahamu jina la Shikalo kama ilivyo sasa. Safari ya Shikalo mwenye miaka 22 kwa sasa, ilianzia katika klabu ya Talanta FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.

Talanta FC iliyomaliza ya saba msimu uliopita ilimsajili Shikalo katikati ya msimu wa 2012 kama kipa mbadala wa George Opiyo aliyetupiwa virago na klabu hiyo msimu huo.

Kuondoka kwa Opiyo kulimpa Samuel Odhiambo fursa ya kuwa kipa namba moja huku usajili mpya wa Shikalo ukiwa ni kama msaidizi wake.

Hata hivyo, alipopata nafasi, Shikalo aliishia kumweka benchi Odhiambo huku kiwango chake kikiisaidia Talanta kumaliza msimu katika nafasi ya pili.

Hata hivyo, Tusker haikusuburi msimu kumalizika ikaamua kumchukua mapema.

Kiwango chake cha nusu msimu tayari kilikuwa kimetosha kumshawishi kocha Francis Kimanzi wakati huo akiifundisha Tusker, kumsajili.

Kimanzi alimsajili Shikalo kama kipa wa akiba baada ya kumruhusu aondoke kipa chaguo la kwanza, Samuel Onyango.

Hii ilikuwa ni baada ya Kimanzi kumsajili kipa Duncan Ochieng kutoka Sofapaka. Na huku akiwa ametibuana na kipa Boniface Oluoch aliyepaswa kusaidiana na Ochieng aliyegoma kurefusha mkataba wake, Kimanzi hakuwa na jinsi ila kusajili Shikalo.

JERAHA LA OCHIENG LAGEUKA KISMATI

Baada ya kuchukuliwa na Tusker 2012, Shikalo alipangwa kwenye mechi tatu pekee hadi mwisho wa msimu huo.

Wiki tatu kabla ya msimu mpya 2013 kuanza, kipa chaguo la kwanza Ochieng akapata jeraha la mkono akiwa mazoezini. Ni jeraha ambalo lilimweka nje kwa zaidi ya miezi mitatu. Hilo likageuka na kuwa bonge la kismati kwa Shikalo.

Ochieng alipata jeraha wakati dirisha la usajili lilikuwa limebakiza siku chache lifungwe, hivyo kocha Kimanzi hakuwa na muda wa kutosha kusaka kipa mzoefu kwani Shikalo na mwenzake Said Dhado walikuwa wangali limbukeni.

Kwa kukosa namna ya kufanya, Kimanzi aliamua kuwatumia Shikalo na Dhado.

Hivyo ndivyo Shikalo alivyoishia kuwa chaguo la kwanza kutokana na kumzidi kiwango Dhado na kuliridhisha benchi la ufundi la timu hiyo.

Baada ya misimu miwili na Tusker, Shikalo alihama na kujiunga na Muhoroni Youth alikodumu kwa msimu mmoja na kujiunga na Postar Rangers. Bandari ilimchukua 2017 ambako nyota yake ilianza kuonekana.

ALIVYOBAMBA

Msimu wake wa kwanza na Bandari ulimfanya kuanza kuangaliwa sana na wachambuzi wa soka hasa wanahabari.

Data zake ziliimarika katika msimu wa 2017/18 alipotuzwa kuwa kipa bora wa msimu, baada ya kuisaidia Bandari kuweka historia kwa kumaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo. Katika msimu huo, Shikalo alimaliza huku akifungwa mabao 17 kutokana na mechi 31. Alikosa tu mechi tatu za ligi msimu huo.

Kwenye msimu wa 2018/19 alibamba tena kwa kuwasaidia Bandari kumaliza wa pili nyuma ya Gor Mahia na pia kutwaa taji la GoTV Shield Cup.

Msimu wa 2018/19 aliumaliza kwa ‘clean sheets’ 14 huku akipenyeza magoli 27 pekee. Msimu huo alihusishwa kwenye mechi zote za ligi isipokuwa ya mwisho dhidi ya Nzoia Sugar.

Kiwango chake pia katika michuano ya Sportpesa Supercup tangu 2018 hadi msimu huu ndio uliowavutia Yanga SC kukazania sahihi yake.

KUHUSU NAMBA PALE STARS

Shikalo ambaye licha ya kusafiri na timu ya taifa Harambee Stars kwa michuano ya AFCON, hakupewa fursa ya kuonja mpira. Lakini licha ya yote hana kinyongo kwani anaamini siku yake itafika huku ya sasa ikiwa ni ya kipa Patrick Matasi ambaye kocha Sebastian Migne kasema ndiye chaguo lake la kwanza.

“Kitu kikubwa zaidi kwa sasa ni mimi kuwepo kwenye timu. Kuhusu namba, sina presha kwa sababu Matasi (Patrick) ndiye kipa mwenye uzoefu mkubwa tuliyenaye kwa wakati huu. Ila kama ikitokea jambo, nipo tayari kujaza nafasi yake na naamini ndio sababu kocha kanijumulisha kikosini. Anafahamu uwezo wangu,” Shikalo alisema.