Sheria ya Bosman inavyowatia jeuri wachezaji wa Simba SC

Tuesday May 14 2019

 

ASILIMIA kubwa ya mastaa wa Simba SC, hasa waliosajiliwa msimu wa 2017/18 wengi wao wakiwa kutoka Azam FC, wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu.

Lakini bahati mbaya kwa klabu yao ni kwamba wengi bado wanaringa kusaini mikataba mipya kwa sababu wanataka kuona AFCON itawawasaidia vipi, kwani wanaweza kufanya maajabu huko na kubadilisha upepo.

Wachezaji hao wana matumaini kwamba yawezekana wakaonwa na mawakala watakaokuwepo huko na ‘kutusua’.

Klabu ya Simba haina cha kufanya maana imeshikwa pabaya...imeshaandaa mikataba yao na ofa ipo mezani, inawasubiri tu wao.

Yawezekana wakawa wanajua au hawajui, lakini kinachowatia jeuri wachezaji hao, na wengine wengi wa klabu nyingine ni sheria ya Bosman ambayo ilianzia Ulaya mwaka 1995.

SHERIA YA BOSMAN

Advertisement

Kabla ya mwaka 1995, klabu za mpira, hasa Ulaya, zilikuwa zikinyanyasa wachezaji. Hata kama mkataba wa mchezaji umeisha, haruhusiwi kujiunga na klabu nyingine yoyote hadi klabu hiyo mpya imnunue kutoka klabu ambayo amemaliza nayo mkataba.

Unyanyasaji huu ulikomeshwa mwaka 1995 baada ya kutungwa kwa sheria ya Bosman iliyoruhusu mchezaji kuwa huru pindi mkataba wake na klabu unapoisha.

ILIVYOKUWA

Jean-Marc Bosman alikuwa mchezaji wa klabu ya RFC ya Ubelgiji ambaye mkataba wake na klabu ulimalizika mwaka 1990.

Mwenyewe hakutaka kuendelea na klabu hiyo, hivyo akapanga kuondoka na kujiunga na klabu nyingine.

Klabu iliyojitokeza kumhitaji ilikuwa Dunkerque ya Ufaransa. Hata hivyo, klabu hiyo ilikataa kulipa dau la Pauni 500,000 ambalo klabu yake ya zamani ya RFC Liege, ilihitaji ili kumuachia moja kwa moja.

Dunkerque ilipokataa kulipa dau hilo, RFC Liege ikamshusha Bosman kutoka kikosi cha kwanza ili kumtia adabu na katika kumkomoa zaidi mshahara wake ukapunguzwa kwa asilimia 70.

Hapo ndipo akaenda kufungua kesi kwenye mahakamani ya Umoja wa Ulaya nchini Luxembourg akiilalamikia Sheria ya FIFA ibara ya 17 ambayo ndio ilikuwa ikitumiwa na klabu.

Kesi hii iliunguruma kwa takribani miaka 5 hadi Disemba 15, 1995 ndipo mahakama ikatoa hukumu.

Katika hukumu yake, mahakama iliamua mfumo uliokuwa ukitumika ulikuwa unavunja makubaliano ya Tume ya Ulaya (sasa ni Umoja wa Ulaya) ibara ya 39(1) inayoruhusu kuhama kwa wafanyakazi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine barani humo.

Bosman na wachezaji wengine wa Ulaya wakapewa uhuru wa kuhama klabu bila malipo yoyote pindi mikataba yao inapomalizika, ilimradi tu uhamisho wao unafanyika ndani ya Ulaya.

MATOKEO YA HUKUMU

Baada ya hukumu hii, klabu zikaanza kuwaheshimu wachezaji na kuanza mapema mazungumzo ya mkataba mpya kuhofia wasije kuondoka bure.

Hapa ndipo vilipoanza vipengele vya bei ya kumuuza mchezaji endapo atataka kuondoka kabla ya kumalizika kwa mkataba wake ‘Release Clause’ na mambo mengine kama hayo.

Lakini pia sheria hii ilizisaidia klabu kwa upande wa mwingine. Kabla ya hapo, klabu zilikuwa haziruhusiwi kuwa na wachezaji zaidi ya watano kutoka nje ya nchi, kwenye mechi moja ya mashindano ya Ulaya.

Sheria iliyotumika iliitwa “three-plus-two” kwamba klabu iliruhusiwa kuwa na wachezaji watatu tu kutoka nje ya nchi yao na wengine wawili kutoka nje ambao wamekulia kwenye akademi ya klabu hiyo.

Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ni mmoja wa waathirika wa sheria ile ya kizamani.

Shirikisho la Soka Ulaya, UEFA, liliwahesabu wachezaji kutoka yale mataifa ndugu na England; ya Wales na Scotland kama wageni wanapocheza England.

Mwaka 1994, Manchester United ilikutana na FC Barcelona kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Kutokana na kubanwa na sheria ile, Ferguson akalazimika kumpanga kipa wa akiba Gary Walsh badala ya kipa namba moja Peter Schmeichel.

Kipa huyo raia wa Denmark aliachwa nje, ili kocha apate nafasi ya kuwapanga wageni Andrei Kanchelskis (Urusi), Denis Irwin (Ireland) na Roy Keane (Ireland) sambamba na ‘wageni wengine’ Mark Hughes (Wales) na Ryan Giggs (Wales). Wakafungwa 4-0 na kutolewa kwenye hatua ya makundi. Lakini sheria hii ilipokuja, wachezaji wote raia wa Ulaya waliruhusiwa kucheza sehemu yoyote ndani ya bara hilo bila pingamizi.

UHURU KAMILI

Bosman akibadilisha upepo wa usajili, kwani hata FIFA iliifanyia mabadiliko ile ibara ya 17 inayohusu sheria juu ya hadhi na uhamisho wa wachezaji.

Kama sio Bosman, mastaa wa Simba wasingeumiza vichwa vya viongozi wao kuhusu mikataba, kusubiri kitakachojiri kwenye AFCON.

Advertisement