Senzo apewa mambo manne Yanga

Muktasari:

Hersi: Tulieni, mbona mambo bado sana

HUKU Simba bado wakimtuhumu kwa kuacha kazi ghafla, Senzo Mazingisa, Yanga wamempa Msauzi huyo majukumu manne mazito ya kufanya ndani ya klabu.

Senzo alikuwa mtendaji mkuu wa Simba kabla ya kuacha kazi juzi Jumapili na jioni yake akatia saini mkataba Yanga ingawa bado hajatambulishwa rasmi.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga, Hersi Said ameliambia Mwanaspoti kuwa ujio wa Senzo katika timu yao ni uthibitisho mwingine watu wa klabu yao kuwa hawakuja kucheza, bali kurudisha nidhamu ya utawala na kuboresha kikosi.

Hersi alisema Senzo kutokana na uzoefu, elimu na rekodi zake kwenye mambo ya soka wameamua kumuajiri kama mshauri wa uongozi wa klabu hiyo inayofumua kikosi chao.

Alisema mbobezi huyo wa masuala ya utawala katika soka hawezi kuwa ofisa mtendaji mkuu wa Yanga kwa vile katiba ya klabu hairuhusu, hivyo atakuwa mshauri mkuu wa uongozi.

Pamoja na mambo mengine, lakini kwanza atahusika kwenye kuusuka upya mfumo wa utendaji wa Yanga ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo wa uwajibikaji wa idara zote. Pili, atahusika kupanga bajeti mbalimbali za klabu huku tatu akitengeneza vyanzo vipya vya mapato ndani ya klabu na nne, atasimamia weledi katika kila jambo linaloihusu Yanga na wadau wake.

Hersi aliongeza kuwa katika mabadiliko ya mfumo wao wa uongozi ambayo wanakwenda kuyafanya ndio maana wamemleta Senzo ili awaongoze kutokana na uzoefu wake kwenye idara hiyo.

“Anakuja kusimama katika kusaidiana na uongozi kwenye mabadiliko ya utawala, hawezi kuwa ofisa mtendaji mkuu kwa kuwa kwa sasa katiba ya klabu hairuhusu kiongozi kama huyo kuwa raia wa kigeni,” alisema Hersi ambaye kampuni yao ndio inayosimamia mchakato wa mabadiliko sambamba na usajili wa Yanga.

Alisema jukumu kubwa ambalo Senzo aliyewapa mataji matatu Simba msimu huu ni kuwajibika kuirudisha kwenye mstari wa weledi na kuisuka Yanga ili ibebe mataji kama ya Simba. “Atakuwa anaushauri uongozi katika kazi zake za kila siku kuanzia kwenye hili la mabadiliko na kuusuka utawala ndani ya klabu.

“(Pia) atakuwa anaushauri uongozi katika kutengeneza bajeti ya klabu - idara zinatakiwa zifanye vipi kazi zake, pia kutafuta vyanzo vya mapato, unajua mpira ni biashara.

“Anajulikana ubora wake, kubwa tunataka aje kusimamia weledi kwenye klabu yetu wengi wanajua tunakokwama kama klabu ndio msukumo umetufanya kumleta Senzo.” Alisema ukiacha mafanikio ambayo ameyapata Simba uzoefu wake katika soka hasa kusimamia weledi ndio hatua kubwa iliyowasukuma kumchukua mara baada ya kuona kuna nafasi ya kumpata. “Mafanikio aliyoyapata Simba yanajulikana, hakuna kigeni lakini ukiangalia mambo ambayo ameyafanya katika klabu mbalimbali alizofanya kazi halafu ukiangalia Yanga tunayotaka kuyafanya utaona hatukukosea kumchukua na nafikiri mengi tutayaongea wakati wa kumtambulisha ukifika,” alisema Hersi na kuongeza kuwa wanaendelea kusajili wachezaji wapya.