Samatta safari ya Temeke hadi Birmingham

Muktasari:

Tajiri wa TP Mazembe, Moïse Katumbi alivutiwa naye kabla ya hata mchezo wa marudiano, April 3, 2011 ambao ulipigwa Dar es Salaam, hakupoa aliendeleza makali yake kwa kuisawazishia Simba bao la pili mambo yakawa 2-2 dakika ya 70 kabla ya kupigwa la tatu.

HATIMAYE ndoto ya nahodha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta (27) ‘Samagoal’ kucheza Ligi Kuu England ‘EPL’ inakwenda kutimia baada ya kukaribia kabisa kujiunga na Aston Villa yenye maskani yake jijini Birmingham.

Imemchukua miaka 12 kupigania ndoto ya kucheza ligi hiyo akiwa kwao Mbagala, Temeke kabla ya hata kujiunga na African Lyon, mwanzoni mwa mwaka 2000, alikuwa akivutiwa na kiwango cha straika wa Arsenal Thierry Henry.

Alijua kusepa na kijiji ndipo hapo shauku ya Samatta, ambaye ni shabiki mkubwa wa Manchester United alipoweka malengo ya kuwa ipo siku, atacheza ligi hiyo ambayo ilikuwa kila wiki akitoa jero lake katika kibanda umiza ili kuifuatilia.

Baada ya maisha ya shule kutokuwa poa, nguvu zake alizielekeza katika soka na hatimaye njia ikafungukia African Lyon ambayo kipindi hicho ilikuwa ikiitwa Mbagala Market, uwezo wake uliifanya miamba ya soka la Ligi Kuu Bara, Simba kumsajili mwaka 2011.

Aliichezea Simba kwa mwaka mmoja tu kufuatia kiwango alichokionyesha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, Machi 20, 2011 ambapo wekundu wa Msimbazi walianzia ugenini nchini DR Congo licha ya klabu yake kupoteza kwa mabao 3-1, alionyesha kiwango cha juu katika mchezo huo.

Tajiri wa TP Mazembe, Moïse Katumbi alivutiwa naye kabla ya hata mchezo wa marudiano, April 3, 2011 ambao ulipigwa Dar es Salaam, hakupoa aliendeleza makali yake kwa kuisawazishia Simba bao la pili mambo yakawa 2-2 dakika ya 70 kabla ya kupigwa la tatu.

Katumbi alikaa chini na viongozi wa Simba na kufanya biashara ya kumsajili Samatta ambako alienda kufanya balaa.

AITEKA AFRIKA

Samatta alikuwa sehemu ya mafanikio ya kikosi cha TP Mazembe ambacho kilitwaa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015, aliifungia miamba hiyo ya DR Congo mabao saba na kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo mikubwa Afrika.

Aliingia TP Mazembe kama mchezaji wa kawaida licha ya kipaji kikubwa alichokuwa nacho lakini aliondoka akiwa mfalme, ilibidi atumie nguvu ya ziada kuondoka maana alikuwa kipenzi cha Katumbi.

Ndani ya misimu minne akiwa TP Mazembe, aliifungia jumla ya mabao 60 katika michezo 103 ya ligi maarufu kama Linafoot.

Samatta alitwaa mataji manne ya Linafoot kwa misimu minne ya 2011, 2012, 2013 na 2013–14, lakini pia alibeba makombe mawili ya DR Congo Super Cup msimu wa 2013, 2014 na lile la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Januari 2016, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Baada ya kubeba tuzo hiyo na kuwepo katika kikosi bora cha mwaka 2015, akatua zake Genk.

AGEUKA MFALME GENK

Jina lake lilikuwa likiimbwa uwanjani Luminus ambao ni nyumbani kwa KRC Genk, alikuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na mchango wake kikosini hapo.

Ndani ya miaka minne akiwa Ubelgiji, Samatta alirejesha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo kwa kukata kiu ya miaka mingi baada ya kuisaidia Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu maarufu kama Jupiler Pro.

Msimu huo wa 2018/19, ulikuwa bora zaidi kwa Samatta kwani alipachika mabao 20, alishika nafasi ya pili katika orodha ya washambuliaji waliokuwa wakikiwania.

Samatta ana tuzo ya kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu Ubelgiji mwenye asili ya Afrika, Ebony Shoe.

Kwa kipindi ambacho ameichezea KRC Genk ni wazi kuwa anastahili kuitwa Lijendi ndani ya klabu hiyo kwani ni mchezaji wa tatu mwenye mabao mengi zaidi katika historia.

Kinara ni Jelle Vossen kwa sasa anaichezea Club Brugge KV (105), Wesley Sonck ambaye amestaafu, Samatta anafuata mabao yake 76.

MAWAKALA WAPISHANA

Samatta ambaye msimu huu ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kucheza na kufunga bao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kiwango chake kiliziweka bize klabu kadhaa barani humo.

Kuna kipindi Brighton, waliripotiwa kutuma wakala wao akamtazame Samatta akicheza. Lazio nayo iliwahi kuhusishwa kufuatilia maendeleo ya straika huyo ambaye msimu huu amefunga mabao 10, yakiwemo matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

YAMETIMIA

Philippe Albert, ambaye ni mchambuzi maarufu wa soka Ubelgiji, aliwahi kutamba akiwa na klabu za Charleroi, KV Mechelen, Anderlecht, alisema kabla ya hata kufunguliwa kwa dilisha hili la usajili Samatta anaondoka Januari.

Isingekuwa rahisi kwa Samatta kuondoka kiangazi kwa sababu ya ushiriki wa Genk Ligi ya Mabingwa, tunajua ukubwa wa mashindano hayo.

Anaondoka wakati ambao kila shabiki wa Genk moyo wake ukiwa mkunjufu, amejijengea ufalme.

Mchambuzi huyo ambaye aliwahi kucheza Ligi Kuu England akiwa na Newcastle United na Fulham, anasema Samatta anaweza kucheza kokote ambako atapata nafasi kutokana na kipaji chake cha kufunga: “Napendekeza akacheze England.”

MAMBO YALISUKWA HAPA

Kampuni ambayo Samatta ameingia nayo mkataba wa kumsimamia mambo yake ya Spocs Consultant, inamsimamia pia staa wa Liverpool, Mohamed Salah.

Pia, inatajwa taasisi yenye soko kubwa nchini England tofauti na ile ya awali ya First For Players.

WASIKIE HAWA

Wachezaji mbalimbali wa Kitanzania, wamemtakia kila la kheri Samatta, ambaye anasubiri muda tu kutambulishwa rasmi na Aston Villa.

Saimon Msuva, ambaye anaichezea Difaa El Jadida ya Ligi Kuu Morocco, alisema Samatta ameendelea kuwa mfano hivyo, kutua kwake England ni ishara ya milango kufunguka kwa Watanzania kucheza ligi hiyo.

“Tangu tukiwa wadogo tumekuwa wafuatiliaji wazuri wa EPL. Kupata nafasi ya kucheza Ligi hiyo sio jambo jepesi, anastahili pongezi na naamini huo ni mwanzo tu, kuna kundi lingine la wachezaji wa Tanzania linakuja,” anasema Msuva.

Msuva ambaye hivi karibuni alikuwa akihusishwa kujiunga na Benfica ya Ureno, anaongeza kwa kusema: “Sina shaka na uwezo wa Samatta, haitokuwa ajabu akiendelea kufanya vizuri akiwa kama ilivyokuwa Ubelgiji.”

Eliuter Mpepo, ambaye anaichezea CD Costa Do Sol ya Msumbiji, anasema: “Siku zote Mungu hamtupi mtu mwenye dhamira ya kweli, Samatta alionyesha nia ya kusonga mbele zaidi na hatimaye milango imemfungukia. Hongera kwake.”

Adi Yussuf, anayeichezea Boreham Wood kwa mkopo akitokea Blackpool ya Daraja la Pili England, anasema wataendeleza kwa pamoja usemi wao wa haina kufeli ambao, wamekuwa wakipenda kuutumia.

“Nimefurahishwa na ujio wake hapa England na atafurahia maisha. Ushindani wa ligi ni mkubwa na kwa uwezo wake atafanya vizuri.

Niliwahi kumshawishi na kutaniana naye kuwa umefika muda wa kuja England, alikuwa akicheka na kusema tusubiri muda sahihi,” anasema Adi.

Upande wake aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ammy Ninje ambaye kwa sasa yupo England, anasema Samatta anaubora wa kumudu mikikimikiki ya ligi hiyo.

“Alionyesha katika mchezo dhidi ya Liverpool tena katika mashindano makubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, namwona kama mkombozi wa Aston Villa kwa sasa.

Anaweza kuchangia sehemu kubwa kuikoa isishuke daraja,” anasema Ninje mwenye taaluma ya ukocha na aliwahi kukiongoza kikosi cha timu ya Taifa, Kilimanjaro Stars kwenye michuano ya Chalenji iliyofanyika nchini Kenya.