Samatta hapa mbona kitawaka

BAADA ya kusimama kwa miezi mitatu, hatimaye Ligi Kuu England maarufu kama EPL inarejea rasmi kuanza kutimua vumbi Jumatano kwa michezo miwili kupigwa kwenye Uwanja wa Villa Park, Birmingham na Etihad huko jijini Manchester.

Pamoja na kuwa bado mapambano dhidi ya virusi vya corona yanaendelea, mataifa makubwa ya soka barani Ulaya, yameamua kurejesha ligi zao za ndani ambazo zilisitishwa kutokana na janga hilo ambalo limeitikisa Dunia.

Mchezo ambao utapigwa Villa Park katika mji wa Birmingham utamhusisha nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akiwa na klabu yake ya Aston Villa ambao wataikaribisha Sheffield United huku muda mchache baadaye Manchester City wakikinukisha dhidi ya Arsenal.

Samatta, ambaye alipata muda wa kufanya mazoezi binafsi ambayo alieleza kuwa yalilenga kujiweka fiti kutokana na ugeni wake England, ana jukumu zito mbele yake kuhakikisha wanajinasua katika hatari ya kushuka daraja.

Kwa mujibu wa ratiba yao, hawa hapa mabeki 10 tishio ambao Samatta ana kibarua cha kukabiliana nao kuanzia Jumatano hadi Julai 26 ambapo, Ligi itafikia tamati.

CHRIS BASHAM

Samatta atakuwa na mtiani mbele yake hiyo Jumatano kutokana na uwezo wa Chris Basham, ambaye amekuwa akitegemewa na kocha wa Sheffield United, Christopher John Wilder kuongoza safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Samatta kukabiliana na beki huyo wa kati, ambaye amekuwa kwa nidhamu katika michezo 28, aliyoichezea timu yake ameonyeshwa kadi nne tu za njano, Basham amekuwa akicheza sambamba na Egan John.

ANTONIO RUDIGER

Kwa mara ya kwanza, Juni 21, Samatta akiwa na chama lake la Aston Villa watawakaribisha matajiri wa London, Chelsea ambayo katika safu yao ya ulinzi wamekuwa wakimtegemea, Antonio Rüdiger kama kiongozi.

Mjerumani huyo ana nguvu na kasi hivyo Samatta anatakiwa kutumia akili ya ziada kumzidi maarifa Rüdiger, ambaye amekuwa akipangwa kucheza na Kurt Zouma au Andreas Christensen au Fikayo Tomori.

JAMAAL LASCELLESS

Juni 24, Samatta akiwa na chama lake watasafiri kwenda St. James Park kucheza dhidi ya Newcastle United ambao katika safu yao ya ulinzi yupo, Jamaal Lascelles ambaye amekuwa akifanya vizuri kama beki wa kati.

WILLY BOLY

Aliwahi kuichezea FC Porto kwa sasa wanafanya vizuri katika kikosi cha Wolverhampton Wanderers, Willy Boly ambaye ni raia wa Ufaransa, amecheza michezo 13 msimu huu wa Ligi Kuu England. Aston Villa itakuwa nyumbani katika mchezo huo, Juni 27.

VIRGIL VAN DIJK

Samatta aliwahi kukabiliana na ukuta wa Liverpool unaoongozwa na Virgil van Dijk wakati akiichezea KRC Genk ya Ubelgiji ilikuwa ni katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na kuwa timu yake ilipoteza katika michezo miwili alifunga bao, Anfield.

Samatta atarejea tena Anfield, Julai 4 wakati huu akiwa na Aston Villa na sio KRC Genk, utakuwa ni wakati mwingine kwake kuendelea kuonyesha makali yake mbele ya beki huyo bora duniani, msimu uliopita alitwaa tuzo ya kuwa mchezaji bora wa msimu.

HARRY MAGUIRE

Ndiye beki ghari zaidi duniani kwa sasa, alitua Manchester United akitokea Leicester City kwa ada ya uhamisho wa Paundi 80 milioni akitokea Leicester City, Samatta atakutana na Harry Maguire, Julai 8 na itakuwa siku ya kipekee kwake kutokana na mapenzi aliyonayo na mashetani hao wekundu wa Old Trafford.

Samatta ana ndoto ya kucheza Manchester United hivyo, hiyo ni nafasi ya kuonyesha makali yake mbele ya ukuta unaoongozwa na Maguire ambaye ndiye nahodha wa timu hiyo.

GARY CAHILL

Alifanya vizuri akiwa na matajiri wa London, Chelsea lakini kwa sasa anatamba akiwa na Crystal Palace, ni beki mzoefu hivyo Samatta anatakiwa kujipanga vilivyo ili kung’ara katika mchezo huo ambao, utachezwa Julai 11, mwaka huu.

MICHAEL KEANE

Julai 15, Aston Villa watakuwa ugenini kucheza dhidi ya Everton ambao kabla ya kusimama kwa Ligi Kuu England wakiwa chini ya Carlo Ancelotti walikuwa wakifanya vizuri huku ukuta wao ukiongozwa na Michael Keane.

DAVID LUIZ

Ni mzoefu ambaye alikuwa akitegemewa timu ya Taifa ya Brazil wakati alipokuwa katika ubora wake kwa sasa kasi yake inaonekana kupungua na ameanza kuwa na mawazo ya kurudi katika klabu yake ya zamani ya Benfica.

Julai 18, Aston Villa wakiwa nyumbani wataikaribisha Arsenal ya Mikel Arteta.

ISSA DIOP

Beki wa kati mwenye asili ya Afrika ingawa ana uraia wa Ufaransa. Ni mhimili mkuu katika safu ya ulinzi ya West Ham United ambayo itavaa na Aston Villa. Ni mtu wa matukio ndio maana anakadi nane za njano. Mchezo huo ambao utachezwa Julai 26 utakuwa wa kumalizia msimu huu wa 2019/20.