Samatta ataka ubingwa Uturuki

Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ambaye ameanza kuonyesha makali yake huko Uturuki amesema kiu yake ni kuhakikisha anatwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo akiwa na Fenerbahce SK.

Samatta ambaye amejiunga na Fenerbahce SK siku chache zilizopita akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu England, amewapa raha mashabiki wa timu hiyo baada ya kuisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Nahodha huyo wa Taifa Stars ambaye alianza kwa mara ya kwanza  kwenye kikosi cha timu hiyo, alifungua akaunti yake ya mabao  nchini humo dakika ya 24 kwa kuunganisha na mguu wake wa kushoto  mpira uliopigwa na nyota wa zamani wa Inter Milan, Caner Erkin.

Samatta aliendelea kuonekana kuwa na njaa ya mabao kwenye mchezo huo kwani dakika ya 67 kipindi cha pili, aliifanya Fenerbahce SK kuongoza kwa wigo wa mabao mawili baada ya kuunganishwa kwa kicha krosi iliyochongwa na mchezaji wa zamani wa Bayern Munich ya Ujeruman, Jose Sosa.

Dakika ya 78, Fatih Karagumruk   walipata bao kwa mkwaju wa penalti lililofungwa na Erik Sabo ambaye hata hivyo alipoteza nafasi nyingine ya mkwaju wa penalti dakika ya 87 wakati huo, Samatta alikuwa amepumzishwa huku nafasi yake akiingia Msenegal, Papiss Cissé.

Cisse naye ni usajili mpya wa Fenerbahce SK, straika huyo ndiye aliyekuwa akitengeza pacha hatari kwenye kikosi cha Newcastle United katika Ligi Kuu England alipotoka Samatta, miaka ya nyuma akiwa na Msenegal  mwenzake  Demba Ba.

Mfungaji huyo wa mabao mawili ya Fenerbahce mara baada ya mchezo huo akiongea na vyombo vya habari vya Uturuki, Samatta alisema, “Nadhani ni mchezo mzuri sana. Mambo yalikuwa magumu kidogo kwetu mwishoni.

Lakini tunafurahi kuwa tumepata alama tatu. Hii ndio muhimu zaidi kwetu. Sasa tunahitaji kuangalia mbele. ”

Samatta aliongea kwa kusema, “Nimefurahi sana kuisaidia timu yangu kwa kufunga mabao. Kama mshambuliaji, lengo langu bila shaka ni kufunga na ninaamini kuwa mabao mengine mengi yanakuja . Timu ni muhimu kila wakati kwangu.

“Ningependelea timu yangu kuwa bingwa kuliko kufunga hata mabao 100 alafu iwe kazi bure. Ninapofunga, ninafurahi kuisaidia timu yangu, lakini kama nilivyosema, jambo muhimu zaidi kwangu ni timu,” alisema.