Samatta ajaza uwanja Fenerbahce

MIAMBA ya soka la Uturuki, Fenerbahce imejizolea zaidi ya mashabiki wapya 80,000 kwenye mtandao wao wa Kijamii wa Instagram ndani ya siku nne tangu wapate saini ya Mbwana Samatta kutoka Aston Villa. Idadi hiyo ya wafuasi ni kubwa kuliko ile ya Uwanja wa nyumbani wa Fenerbahce, Sukru Saracoglu unaojaza mashabiki wapatao 50,509.

Septemba 25, 2020, Samatta alitangazwa kujiunga na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki maarufu kama ‘Super League’ kwa kusaini mkataba wa miaka minne.

Kitendo cha Aston Villa kuamua kumuonyesha mlango wa kwaheri Samatta kilipokelewa tofauti na Watanzania ambao, waliamua nao kuanzisha kampeni za kuihama klabu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii hasa Instagram.

Ndani ya saa 24 tangu watangaze rasmi kuachana na Samatta huku wakimtakia kila kheri, walijikuta wakipoteza zaidi ya wafuasi 25,000, idadi hiyo iliendelea kuongezeka.

Kabla ya Fenerbahce kumtambulisha Samatta kuwa mchezaji wao huku akipewa jezi namba 12 kabla ya baadaye kubadilishiwa na kupewa 10, walikuwa na wafuasi 5,653, 638.

Idadi ilikuwa ikiongezeka kwa kasi hadi jana asubuhi walikuwa tayari wamepata wafuasi wapya 89,672.

Idadi ya wafuasi wapya wa Fenerbahce huku wengi kwenye takwimu hizo wakiwa ni Watanzania ni kubwa kuliko hata idadi ya mashabiki ambao wamekuwa wakipaswa kuingia kwenye uwanja wa klabu hiyo licha ya kuwa kwa sasa kuna katazo la kuingia uwanjani kutokana na corona.

Sakata la Samatta limewafanya wadau mbalimbali wa soka duniani kukumbuka kile ambacho kilitokea kwa Cristiano Ronaldo na klabu yake ya zamani ya Real Madrid ya Hispania wakati akijiunga na Juventus ya Italia.

Kitendo cha Ronaldo kusepa Madrid kiliwafanya kupoteza mashabiki milioni moja ndani ya saa 24 huku Juventus wakijizolea Cristiano Ronaldo wafuasi wapya milioni 4.7.