Samatta aipa neno Taifa Stars

Wednesday November 13 2019

 

By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta amesema wachezaji wamebeba dhamana ya kuifunga Guinea ya Ikweta, Ijumaa wiki hii.

Samatta alitoa kauli hiyo muda mfupi kabla ya klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji kumtimua kocha wake Felice Mazzu baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha msimu huu.

Timu hizo zitavaana katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa moja usiku.

Akizungumza jana, Samatta alisema ana imani na mbinu za benchi la ufundi na jukumu la kuamua matokeo limebaki kwa wachezaji hasa wanaocheza soka nje ya nchi.

Pia alisisitiza asingependa kuona Taifa Stars ikishindwa kutumia vyema mechi za nyumbani kupata ushindi akitolea mfano mechi ya kufuzu fainali hizo dhidi ya Lesotho mwaka juzi.

“Sisi ndio tuna dhamana ya kuamua mechi na Guinea, sitafurahi kuona yale ya Lesotho yakijirudia. Tulitumia nguvu kubwa katika mechi ya mwisho na Uganda wakati tulikuwa na nafasi ya kuifunga Lesotho Dar es Salaam,”alisema Samatta.

Advertisement

Katika mchezo huo Taifa Stars ililazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa kabla ya kufungwa 1-0 ugenini. Timu hiyo iliifunga Uganda mabao 3-0 Dar es Salaam na kufuzu fainali hizo kwa mara ya pili.

Samatta alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuwasili nchini akitokea Ubelgiji anakocheza soka ya kulipwa. Katika safari yake nyota huyo aliongozana na Simon Msuva anayecheza katika klabu ya Difaa Al Jadida ya Morocco.

Samatta alisema haifahamu Guinea ya Ikweta, lakini ana matumani na kikosi chao hasa wachezaji wanaocheza nje kwa kuwa wamepata uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa.

Wachezaji wanaocheza nje ni Hassan Kessy (Nkana, Zambia) Eliuter Mpepo (Buildcorn,Zambia), Farid Mussa (CD Teneriffe, Hispania), David Kissu (Gor Mahia, Kenya).

Fainali za Kombela Mataifa Afrika mwakani zimepangwa kuchezwa nchini Cameroon. Taifa Stars imepangwa Kundi J na timu za Libya na Tunisia.

Advertisement