Samatta abebeshwa jukumu la ubingwa Genk

Wednesday May 15 2019

 

By Eliya Solomon

MBONGO aishie Ubelgiji, Jeff Megan amesema mashabiki wa KRC Genk anayoichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ wamejawa na mchecheto wa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo ‘Jupiler Pro’.

Megan ambaye amekuwa na ukaribu na Samatta, alisema matumaini ya mashabiki wa timu hiyo, wanaamini Samagoal aliyewafungia mabao 23 kwenye Ligi, anaweza kufanya mambo kwenye michezo yao miwili iliyosalia.

“Pamoja na kuwa tulipoteza kwenye mchezo muhimu  dhidi ya Club Brugge kwa mabao 3-2, wengi hatukuumizwa na matokeo yale kutokana na wachezaji wetu walivyojituma.

“Mchezo unaokuja nao tutakuwa ugenini dhidi ya Anderlecht, imani ya wengi ni kwa Samatta, amekuwa kwenye kiwango bora hivyo ushindi utatuweka pazuri,” alisema Megan.

Kutokana na utofauti wa pointi tatu uliopo kati ya KRC Genk ambao ni vinara wa Ligi ndogo ‘Play off’ wakiwa na pointi 50 na Club Brugge (47), chama la Samatta wanahitaji pointi nne kwenye michezo yao miwili iliyosalia ambayo ni dhidi ya Anderlecht,kesho, Alhamisi  na Standard Liège, Jumapili Mei 19.

Endapo wakina Samatta kesho watashinda na Club Brugge wakipoteza hapo kesho mbele ya  Standard Liège  basi, KRC Genk watatangazwa kuwa mabingwa wapya wa  Jupiler Pro kwa msimu huu wa 2018/19

Advertisement

Advertisement