Said Ndemla alivyoichunia Yanga, Stars yampa nguvu

Monday October 12 2020

 

By CLEZENCIA TRYPHONE

UKITAJA viungo tano bora wazawa hapa nchini jina la Said Ndemla haliwezi kukosa ndani yake kutokana na uwezo wake wa kusakata kabumbu aliotunukiwa na mwenyezi Mungu.

Mbali na kuonyesha uwezo msimu huu katika michezo mitano, mitatu ameanza kikosi cha kwanza huku mmoja akitokea benchi, ameweza kujumuishwa ndani ya kikosi cha nyota 25 wa Taifa Stars kilichocheza jana dhidi ya Burundi.

Mwanaspoti imefanya mahojiano maalum na Ndemla ili kujua maisha yake ya soka Simba, uvumilivu aliokuwa nao ndani ya kikosi hicho licha ya kukosa namba huku akishindwa kwenda Yanga baada ya kutajwa kujiunga katika dirisha kubwa la usajili hivi karibuni.

SIRI YAKE SIMBA

Anabainisha kuwa Simba ni timu ambayo imemfanya ajulikane mpaka leo anakubalika kutokana na uwezo wake, hivyo kukaa kwake benchi na maamuzi yake ambayo hayakupaswa kuingiliwa.

“Nilikuwa naona sana katika mitandao ya kijamii kila mtu Ndemla, Ndemla lakini niliamua kukaa kimya nione mwisho wake, sasa hivi wamenyamaza,”

Advertisement

“Mimi ni mtu mzima najua nini nakifanya, kumbuka ndani ya timu tunakuwa wachezaji wengi, sasa kocha akiona anafaa kuanza fulani mwingine unasubiri na muda ukifika unacheza tu.”

Ndemla anabainisha kuwa, maneno ya mitandaoni ukiyatilia maanani unaweza kushindwa kucheza mpira, hivyo aliamua kuziba masikio.

Anasema anafurahia maisha yake ndani ya Simba kwa kuwa ni timu ambayo imemlea toka akiwa timu ya vijana miaka 10 iliyopita na sasa timu ya wakubwa ambayo anaimani itamvusha alipotarajia kufika.

KUTOKA NJE YA SIMBA

“Wakati ndio kila kitu, unaweza ukataka kuwahi kumbe wakati wako unakuwa haujafika, na unapokuwa mvumilivu kila kitu kinaenda sawa,”anasema.

Anasema wakati utakapofika ataondoka Simba tena kwa heshima kwenda timu nyingine iwe ndani au nje ya nchi akiamini kila kitu ni mipango ya Mungu.

“Mungu ndiye anapanga nini kitokee hata mimi kuna ofa nyingi nazipata lakini nashindwa kwenda hiyo yote ni mipango ya Mungu tu lakini kuna siku utasikia Ndemla nimeondoka.”

MALENGO YAKE SASA

“Kwanza niisadie Simba izidi kutwaa mataji na pia nafasi yangu ndani ya Taifa Stars iweze kuzaa matunda, hayo ya kwenda kucheza soka nje ya nchi yanakuja tu, naimani nako nitafika, uwezo na nia ninayo”

CHANGAMOTO

“Changamoto zipo nyingi sana, ila ukiwa na hasira mpira unaweza kukushinda kucheza, nilipokuwa benchi nilikumbana na changamoto nyingi sana, unasemwa hata na usiyemjua lakini niliikubali hiyo hali maisha yakaendelea,”

Katika maisha ili uweze kusonga mbele changamoto ni lazima ukumbane nazo alafu unazivumilia ili maisha yaweze kusonga mbele na ndicho alichokifanya Ndemla.

VITA YA NAMBA

“Nakabiliana nayo na nimeweza kuikabili, uvumilivu kwangu ndio silaa sasa hivi napata nafasi na maisha yanaendelea, hata waliokuwa wakinisema sasa hivi wamenyamaza,”

Anasisitiza kujituma zaidi ili kuendelea kulinda kiwango chake ndani ya timu ili azidi kuaminika chini ya kocha wake Mkuu Sven.

MWANAE KURITHI

Anabainisha kuwa hatohitaji mwanae kufuata kipaji kama chake na atamtaka kufanya mambo mengine nje ya mpira kwa kuwa kila kitu anakijua na amekiona.

“Sitaweza kumruhusu mwanangu kucheza mpira, nitapambana kama baba ili nimpe urithi wa elimu ambao naimani ndiyo funguo ya maisha yake.”

LIGI KUU 2020/21

Asilimia kubwa ya wachezaji wameizungumzia ligi msimu huu kuwa ngumu na yenye ushindani kutokana na kila timu kujipanga na kuhitaji matokeo katika kila mchezo.

“Ligi ni ngumu sana, kila timu ukikutana nayo iwe nyumbani au ugenini wachezaji wanakaza kupata matokeo, itakuwa ligi nzuri yenye ushindani mkubwa tofauti na misimu uliyopita,”

KUIKACHA YANGA

Wakati wa dirisha kubwa usajili kuelekea msimu huu, Ndemla alitajwa kutua Yanga lakini mwisho wa siku mabosi wa Msimbazi wakamuongezea kandarasi ya miaka miwili mpaka msimu wa 2021/22.

“Hata nilikuwa naona katika vyombo vya habari kuwa Ndemla anaenda Yanga, zilikuwa habari tu sikuwahi kuongea nao juu ya ofa ya kunitoa Simba zilikuwa habari tu za watu na maslahi yao,”

“Nilikuwa nashangaa lakini naujua vizuri mpira wa hapa bongo hata sipati tabu.”

KIBOKO YAKE

Katika mafanikio aliyokuwa nayo nyota huyo, anasema hawezi kuacha kutoa shukrani kwa Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu kwa kuwa ni moja ya watu wake wa karibu ambao wanamshauri mambo mengi yanayomfanya asikate tamaa.

Mbali na huyo pia anatambua mchango wa Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ , Seleman Matola pamoja na Abdallah King Kibadeni, kwani hao nao ni moja ya watu wanaomtakia mema katika kandanda.

KUITWA STARS

Ndemla ni moja ya viungo walioitwa na Kocha Mkuu wa Stars Etienne Ndayiragije kuelekea mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki unaotambuliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA dhidi ya Burundi uliopigwa jana na Tanzania kufungwa bao 1-0.

Anasema kuitwa kwake ndani ya kikosi hicho kumezidi kumpa nguvu na morali zaidi ya kujua bado anathaminika na uwezo wake unaonekana hivyo hatomuangusha aliyemuona anafaa na kumuita.

“Wachezaji tuko wengi sana, kitendo cha mimi Ndemla kuwa miungoni mwa wachezaji 25 sio jambo dogo ni kitu kikubwa sana kwangu mimi, nitapambana kadri ya uwezo wangu kuhakikisha naisaidia timu yangu katika mechi zote ambazo nitapata nafasi ya kuitwa,”

“Mimi nilishacheza timu ya Taifa ila hivi karibuni kutokana na changamoto za hapa na pale sikuweza kupata nafasi hiyo, na ndio maana toka mwanzo nimesema tatizo ni wakati ukifika tu kila kitu kinaenda sawa,”

ANAYEMZIMIA

Karata yake namba moja anaitupa kwa kiungo mwenzake wa JKT Tanzania Mwinyi Kazimoto aliyewahi kucheza Simba pia.

“Mwinyi yule jamaa fundi sana, anajua nini anakifanya awapo ndani ya dimba, namkubali sana, na nilikuwa napenda kumtizama awapo na mpira dimbani, yuko vizuri sana huyu jamaa,”anasema Ndemla aliyewahi kucheza Soccer Rangers ya Magomen pamoja na Linea Messina na ndio Simba walipomnasa.

Anasema anafarijika anapokuwa na vijana wenzake aliotoka nao Simba B Ibrahim Ajib pamoja na Jonas Mkude.

Advertisement