Sababu za kipigo Taifa Stars ni hizi

Muktasari:

Baada ya kikosi cha Timu ya Taifa Stars kupokea kipigo cha mabao 3-0, kutoka kwa Cape Verde, wataalamu wa soka wameuzungumzia mchezo huo kwa kueleza sababu ya kufungwa na kinachotakiwa kufanyika katika mechi ya marudiano, itakayochezwa wiki ijayo.

KIKOSI cha timu ya Taifa kimerejea nchini kutoka Cape Verde kikiwa na machungu ya kipigo cha mabao 3-0 ilichopewa na wenyeji wao, katika mechi ya kuwania fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zitakazofanyika Cameroon. Kipigo hicho cha ugenini kimeiweka Stars katika nafasi ngumu ya kuipata tiketi ya fainali hizo za mwakani, salama yake ni kushinda mchezo wa marudiano dhidi ya wapinzani wao hao keshokutwa Jumanne.

Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya makocha na wachambuzi kilichoiponza Taifa Stars kwenye mchezo huo wa usiku wa juzi mjini Praia na kipi kifanyike kwa mechi yao ya marudiano jijini Dar es Salaam.

MAANDALIZI MABOVU/ UCHOVU

Mchambuzi wa michezo na nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay anasema hakukuwa na maandalizi mazuri ya kucheza na Cape Verde kiufundi, kimbinu hata kiutimamu wa akili na nguvu.

“Inaonekana timu ilifanya maandalizi ya kucheza na Cape Verde bila kuwajua. Inadaiwa hata katika maandalizi ya Stars hapa nyumbani walijiandaa zaidi kwenye ‘fiziki’ lakini wachezaji hao wanatoka kwenye klabu zao na wamefanya mazoezi mazito jambo lililowafanya wawe wachovu.”

Jambo hilo liliungwa mkono na Kocha wa Yanga, Mcongo Mwinyi Zahera aliyesema, uchovu ulichangia Stars ipate matokeo hayo ya aibu na kipigo cha kwanza cha Kocha Emmanuel Amunike anayeinoa timu hiyo.

“Mzunguko wa safari ulikuwa mkubwa ndiyo maana wakacheza kwa uchovu, nilishangaa sana kuona TFF inaruhusu wachezaji wa Stars kutoka kambini kwenda kuzitumikia klabu zao na wengine nimesikia wameumia. Hii si sawa,” alisema Zahera.

MFUMO/ BEKI

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alikiri aliufuatilia mchezo huo kwa njia ya runinga mwanzo mwisho na kubaini beki ya Stars haikucheza vizuri kwani Aggrey Morris, Hassan Kessy na David Mwantika hawakuwa katika ubora wao.

Alisema, huwezi kumlaumu Amunike hata katika suala la kutomchezesha Kelvin Yondani ‘Vidic’ na kuhoji kwa nini Mwantika anacheza ni kwa sababu alifanya vizuri mechi dhidi ya Uganda mjini Kampala na matokeo kuwa suluhu.

Mayay alifafanua juu ya suala la mbinu zilizotumika, hazikuwa nzuri kwani katika mfumo walicheza kujilinda zaidi jambo lililowapa nafasi Cape Verde kushambulia mara kwa mara:

Alisema kuanza kwenye kiungo na Himid Mao na Mudathir Yahya ambao ni kama viungo wakabaji kuliifanya timu iwe nyuma ndio maana muda mwingi Mbwana Samatta alikuwa akifuata mipira na kwenda nayo mbele na kujikuta akichoka haraka.

HATUWAWEZI

Mwaisabula alishindwa kujizuia na kusema; “Pamoja na mambo yote, tukubali kuwa, Cape Verde wanatuzidi kwenye soka, ndio maana wao wako nafasi ya 67 kwenye viwango vya Fifa na sisi tuko 140. Hata kama unawaona wanacheza tu, ndiyo staili yao. Ndiyo maana wako hapo.”

Upande wa Afrika, Cape Verde inashika nafasi ya 13 na Tanzania ya 38, huku Tunisia ndio vinara na Mwaisabula alisema sehemu kubwa ya wachezaji wao wako nje ambao ni zaidi ya 17 na Tanzania ndiyo kama wanaanza.

“Sisi tunajifunza, bado tunafanya makosa na kurekebisha hivyo lazima tukubaliane jambo hilo wametuzidi.”

SAMATTA HASTAhILI

Mwaisabula alisema kitendo cha kumchezesha Mbwana Samatta nyuma, atoke kwenda kutafuta mipira ya kufunga nje ya 18, ni tatizo.

“Amunike anakosea namna ya kumchezesha Samatta, alitakiwa amwache acheze mtu wa mwisho na kazi yake iwe kusubiri mipira na kufunga tu lakini si kutoka,” alisema Mwaisabula na kuongeza. “Endapo atacheza nafasi ya mshambuliaji wa mwisho, mipira ya kufunga itafika tu hata ikiwa mitatu kati ya hiyo, miwili au mmoja atafunga.”

NINI KIFANYIKE?

Mwaisabula alisema, anatarajia kuona Stars itakayocheza mechi ya marudiano na Cape Verde kuwa na mabadiliko makubwa hasa eneo la ulinzi baada ya makosa hayo kuonekana mjini Praia.

“Kocha yeyote anapoona timu imepoteza lazima kuna upungufu na yanatakiwa kufanyiwa mabadiliko kama hivyo kwenye ulinzi kuisuka upya na ushambuliaji kwa Samatta kama nilivyosema.”

Alisema ni jukumu la kusahau matokeo hayo na kujipanga upya na Watanzania wawaombee.

Kwa matokeo ya juzi, Stars imerejea mkiani ikiipokea Cape Verde katika Kundi L lenye timu za Uganda na Lesotho ambazo jana Jumamosi zilikuwa uwanjani zikiumana mjini Kampala baada ya kusaliwa na alama zao mbili na bao moja.

Uganda ilikuwa kileleni ikilingana alama 4 na Cape Verde (kabla ya mechi yao ya jana) wakitofautiana mabao na kufunga na kufungwa huku Lesotho ikiwa ya tatu na alama mbili kama Tanzania ila ikibebwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mara ya mwisho Stars kushiriki fainali za Afcon ni mwaka 1980 nchini Nigeria na michuano mikubwa mingine iliyofuzu ni Chan 2009 iliyofanyika Ivory Coast kipindi timu hiyo ikinolewa na Mbrazili Marcio Maximo aliyemaliza mkataba Julai 2010 na kwa kiasi fulani aliisaidia timu hiyo.