SIO ZENGWE: Tuanze kufanya tathmini ya ligi pamoja

Monday July 20 2020

 

By ANGETILE OSIAH

MSIMU wa soka unakaribia kufika kileleni baada ya mwaka huu kulazimika kuisha Julai kutokana na mlipuko wa virusi vya corona ulioikumba dunia nzima.

Ulitukuta tukiwa hatujajiandaa vizuri kukabiliana na majanga ya aina hiyo, hivyo haistahili kutupiana lawama kwa lolote lililokwenda vibaya kutokana na mlipuko huo.

Jambo moja ambalo nimeona ni fundisho baada ya mlipuko huo ni kurekebisha kanuni zetu ili zitarajie jambo kama hilo huko mbeleni na hivyo kuweka jawabu la nini kifanyike.

Hapa simaanishi wahusika waende kurekebisha kanuni na kuweka mstari mmoja tu “Iwapo kutatokea janga, timu inayoongoza ligi ipewe ubingwa”.

Najua kunaweza kuwa na haraka kama hizo, lakini si suala la kukaa siku moja na kuongeza hiyo sentensi na kutangaza.

Suala hilo linahitaji majadiliano ya kina na kuliangalia kwa mtazamo mpana zaidi ili kupata jawabu sahihi linalolingana na mazingira yetu na mahitaji ya huko nje, ambako huwa tunashiriki mashindano mengine.

Advertisement

Lakini leo nilitaka kuzungumzia zaidi tathmini. Najua TFF huwa na tathmini ya msimu uliopita ambayo huisaidia kufanya marekebisho katika kanuni zake na masuala mengine.

Lakini kadri mahitaji ya mpira yanavyokuwa makubwa, ni muhimu kukawa na tathmini pana zaidi itakayohusisha wadau wengi wote ili kuangalia uendeshaji kwa ujumla, miundombinu, uamuzi, udhamini, mapato, masoko, soka la vijana, la watoto na la wanawake na ukubwa wa mashindano.

Najua sehemu fulani ya vitu kama hivi imekuwa ikifanywa na shirikisho lenyewe, lakini kuna haja ya kupanua wigo ili kupata maoni tofauti kuhusu mpira wetu, hasa ikitiliwa maanani kuwa taasisi na watu binafsi wanatumbukiza fedha zao kwa matarajio ya kuendeleza biashara zao, huku mashabiki wakiweka fedha kwa matarajio ya kuona burudani na bingwa kupatikana kwa haki.

Lakini uwekezaji katika ligi yetu kubwa bado ni mdogo, hivyo katika ligi za chini ndio hali mbaya kabisa.

Tunahitaji wadau watueleze nini kifanyike ili washawishike kuwekeza zaidi katika soka isiwe kama ilivyo sasa kwa wanaoweka fedha kuona kama wanafanya hisani au fadhila.

Tunahitaji kujua nini kinatakiwa kifanyike.

TFF hujaribu kutoa mafunzo kwa watendaji wa klabu, lakini wahusika hutuma maofisa habari ambao hawajui lolote kuhusu uendeshaji wa klabu na hivyo mafunzo hayo kupotea bure.

Kwa hiyo linahitajika jukwaa la viongozi au wamiliki wa klabu, wawekezaji, wadhamini na wandeshaji mpira kukutana pamoja ili kueleza nini kinatakiwa kifanyike na maazimio yanaweza kuingizwa katika sharia au kanuni za uendeshaji kwa ajili ya msimu unaofuata.

Tathmini hiyo haitakiwi iishie kwa viongozi, wadhamini na wandeshaji ligi tu, bali hata kwa wataalamu wenyewe wanaofundisha wachezaji wetu.

Kuna Chama cha Makocha wa Soka (Tafca) ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

Hawa nao hawana budi kuwa na tathmini yao ya msimu mzima na kutoa ripoti ya kiufundi katika jukwaa la makocha na wataalamu wengine na kujadili ili kutoa mapendekezo yao kuhusu mafanikio na matatizo ya ufundishaji kwa jumla, makocha na masuala mengine na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kwa waendeshaji mchezo.

Hata Chama cha Wanasoka (Sputanza) kina wajibu wa kuwa na tathmini yao ya kiufundi ya mwaka ambayo itaeleza mafanikio na matatizo ya wachezaji na kutoa mapendekezo yao ambayo yanaweza kuingizwa katika sharia au kanuni za soka ili kuwawekea mazingira mazuri zaidi wachezaji.

Kwa kawaida tathmini ndiyo hutuonyesha tulifanya nini kwa kipindi fulani, tulifanikiwa wapi ili tupaimarishe na tulikosea wapi ili tuparekebishe. Zaidi ya hapo, huonyesha tulikosa nini ili tuingize kitu hicho.

Hii itaondoa kufanya mambo ili mradi. Najua hapa tatizo kubwa litakuwa ni gharama za uendeshaji wa vikao hivyo vya tathmini. Lakini penye nia pana njia.

Advertisement