SIO ZENGWE: Madaktari nao walikuwa likizo ya corona?

Moja ya vitu vine muhimu katika michezo, na hasa soka ni tiba ya michezo. Ni suala ambalo halitakiwi kuwa kando ya mjadala wowote kuhusu uendeshaji mpira wa miguu na maendeleo yake.

Kusahau masuala ya afya ni sawa na kukubali kuacha mguu mmoja uondoke na bado unataka kufika sehemu unayokwenda, kwa haraka. Ni lazima kasi yako itaathirika na hutafikia malengo kikamilifu kwa kuwa hukwenda kikamilifu.

Ndivyo ambavyo masuala ya soka yanatakiwa kujadiliwa. Ukamilifu katika soka au michezo mingine, unakuwepo pale suala la afya na tiba ya wanamichezo linapozingatiwa kikamilifu.

Ndio maana kanuni za michezo yetu zinazungumzia afya na kulazimisha kila klabu kuwa na daktari wa michezo kwa ajili ya mambo mengi, kuzingatia afya wakati wa kupanga program za mazoezi, kutoa hata ushauri kwa aina ya chakula, kutoa tiba zisizohitaji mchezaji kupelekawa hospitali kama kushauri kuhusu uchuaji misuli.

Katika timu, kunaweza kuwa na daktari wa timu (TD) ambaye anaongoza jopo la wahudumu wa afya wa nyanja tofauti, lakini katika hizi timu zetu, mtu huyo atabeba majukumu mengi kama kushughulikia majeraha, maradhi, kushauri kuhusu kujikinga na maradhi na majeraha, huduma ya dharura, masuala ya hali ya hewa, uchovu wa safari za ndege, dawa zinazozuiwa michezoni na kuongeza kiwango cha wachezaji kwa kula chakula sahihi.

Kwa hiyo, huwezi kuona sehemu ambayo uongozi unazungumzia mipango ya timu bila ya kumuhusisha au shirikisho likizungumzia mipango ya maendeleo bila ya kuihusisha kamati ya tiba.

Ndivyo ilivyotakiwa kuwa wakati huu ambao tulikuwa tukijadili mapumziko ya dharura yaliyotokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.

Yaani badala ya viongozi wa klabu na makocha kusikika kila siku, zilitakiwa zisikike sauti za madaktari wa timu wakieleza jinsi kipindi cha mapumziko kingetumiwaje ili wachezaji wanaporudi wawe katika utimamu wa mwili.

Ndicho kipindi ambacho madaktari wa timu wangezungumzia umuhimu wa aina ya vyakula ambavyo wachezaji walitakiwa watumie wakati wa mapumziko hayo. Ndicho kipindi walitakiwa wazungumzie kwa nini ugonjwa huo si hatari au ni hatari kwa wanamichezo, kama Dk Wilhelm Bloch wa Ujerumani alivyoonya kuwa wachezaji wako hatarini kustaafu soka iwapo watapata maambukizi.

Alisema pamoja na ukweli kwamba miili, mfumo wa kinga na mfumo wa mishipa ya damu ya wachezaji inamaanisha kuwa hatari kwao ni ndogo, lakini haijajulikana kama maambukizi madogo hayasababishi kuharibika kwa mapafu, hali ambayo inaweza isipone kabisa au kuchukua muda mrefu kurudi katika hali ya kawaida.

Tulitegemea madaktari ndio watuambie hali itakuwaje katika mazingira ambayo wachezaji walioagizwa kufanya mazoezi tofauti wakati wa kipindi cha likizo ya dharura wataweza kustahimili mechi za dakika tisini (Fifa imeongeza idadi ya wachezaji kubadilishwa), tena ambazo zitakuwa vituoni kwa raundi zote zilizosalia.

Hawa ndio ambao wangewasilisha mikakati ya nini Shirikisho la Soka (TFF) linatakiwa lizingatie na kupeleka serikalini kama mkakati wake wa kuzingatia afya za wachezaji wakati michezo itakapoanza tena mwezi ujao huku Covid-19 ikiendelea kuwepo.

Tungesikia jinsi klabu zao zilivyojipanga kwa ajili ya kurejea kwa michezo—yaani kupendekeza upimaji, muda wa mechi kuanza, malazi kwa wachezaji ambao kwa kawaida huwa wawili katika kila chumba, hofu na matarajio yao.

Hata vyombo vya habari vimekuwa vikitafuta viongozi na makocha zaidi badala ya watu hawa muhimu katika kipindi cha corona. Kwa kuwa viongozi wanataka mechi zichezwe, na hali kadhalika makocha, huwezi kusikia maoni tofauti kuhusu afya za wachezaji katika kipindi cha mlipuko wa corona kwa kuwa wenye taaluma hawaongei.

Sijui ni kwa nini waliamua kutotumia fani yao kuibua hoja kadhaa kuhusu wanamichezo na corona.