Rio amwambia Ole Gunnar hii sasa ni aibu Man United

Muktasari:

Katika muongo uliopita, mara mbili tofauti Man United ilivuna pointi chache baada ya mechi 24 ilikuwa pointi 40, walipokuwa chini ya David Moyes 2013/14 na Louis van Gaal 2015/16. Lakini, msimu huu hali ni mbaya zaidi, timu imevuna pointi 34 tu katika mechi hizo 24.

MANCHESTER ,ENGLAND . MASHABIKI wa Manchester United wamechoka na sasa wanamtaka kocha Ole Gunnar Solskjaer afutwe tu kazi baada ya timu kukumbana na kipigo kingine cha aibu.

Mashabiki hao walivumilia baada ya kuchapwa 2-0 na Liverpool Jumapili iliyopita, hawakuumia sana kwa sababu ya ubora wa wapinzani wao na tena walikuwa Anfield, lakini kupigwa tena 2-0 tena nyumbani Old Trafford, tena na Burnley kumewauma zaidi mashabiki hao huku Solskjaer mwenyewe akiweka rekodi ya kufungwa mara nyingi kuliko mechi alizoshinda tangu alipochukua mikoba ya jumla ya kuinoa timu hiyo Machi mwaka jana.

Katika mchezo huo pia wamewashuhudiwa Burnley wakiweka rekodi yao ya kupata ushindi wa kwanza Old Trafford tangu mwaka 1962, huku wakiwaumiza zaidi Man United kwa maana ya kwamba Burnley imeshinda mechi nyingi kuliko wababe hao wa Old Trafford tangu walipoanza kuwa chini ya Solskjaer. Man United imeshinda mechi 11 za Ligi Kuu England chini ya Solskjaer, lakini wamefungwa 12 na kutoka sare tisa katika mechi 32 ambazo bosi huyo wa zamani wa Cardiff City na Molde ameiongoza.

Katika muongo uliopita, mara mbili tofauti Man United ilivuna pointi chache baada ya mechi 24 ilikuwa pointi 40, walipokuwa chini ya David Moyes 2013/14 na Louis van Gaal 2015/16. Lakini, msimu huu hali ni mbaya zaidi, timu imevuna pointi 34 tu katika mechi hizo 24.

Rekodi za Solskjaer ni za hovyo kuliko hata za mtangulizi wake Jose Mourinho, ambaye aliondolewa na yeye kupewa nafasi. Mourinho, ambaye alifutwa kazi Desemba 2018, yeye alishinda mechi 17, sare 12 na vichapo vitatu tu katika mechi zake 32 za kwanza kwenye ligi akiwa na wababe hao wa Old Trafford. Hiyo ni sawa na wastani wa ushindi wa asilimia 50, wakati Solskajer ushindi ni asilimia 34 tu.

Mashabiki wa Man United kwenye mchezo huo wa juzi usiku waliimba nyimbo za kuwaponda pia Ed Woodward na familia ya wamiliki, Glazers.

Baada ya hapo walihamia huko kwenye mitandao ya kijamii na kumshambulia Solskjaer, ambapo mmoja aliandika kwenye Twitter: “Habari za asubuhi. Ni saa 1 asubuhi na bado sijasikia habari za Solskjaer kufukuzwa. Hii ni siku mbaya kwangu.”

Mwingine aliandika: “Solskjaer anapaswa kufukuzwa na sio kuendelea kumshikilia huyu mpuuzi.”

Hilo la mashabiki linaonekana kumgusa beki wa zamani wa timu hiyo, Rio Ferdinand ambaye pia amepoteza imani na Solskjaer na kueleza kwamba matokeo ya Man United, hayafurahishi kwa kusema ukweli.

Beki huyo wa zamani wa Old Trafford kwa muda mrefu alikuwa mtetezi wa Solskjaer na kupiga sana debe la kumtaka apewe kazi baada ya kufanya vizuri alipokuwa kocha wa mpito, kwa sasa mambo yanaonekana kugeuka, hata yeye amechoka.

Rio aliulizwa kama Solskjaer anastahili kubaki kwenye kibarua chake, alisema: “Matokeo hayasemi hilo. Nilicheza na Ole, ni mchezaji mwenzangu wa zamani, lakini haya matokeo yapo wazi, sio mazuri kabisa.”

Ferdinand aliongeza: “Nitamsapoti Ole kwa jambo moja tu, kuwa na majeruhi wengi wachezaji wake muhimu. Yule McTominay alikuwa vizuri sana kabla hajaumia.

“Pogba ni mchezaji mkubwa, mchezaji ghali kwenye timu. Na Rashford ameumia akiwa kwenye kiwango chake bora. Hivyo ana wachezaji wake muhimu wote majeruhi. Hata hivyo ana pesa nyingi anapaswa kusajili. Ona timu sasa inamtegemea mtoto wa miaka 18 aingie wakati wa mapumziko kubadili mambo, kweli hiyo ni Manchester, tumefika hapo.”

Man United wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuvuna pointi 34 katika mechi 24 walizocheza, ambapo wameshinda tisa, sare saba na vichapo vinane, huku wakiwa na mabao 36 ya kufunga na kufungwa 29.