Rich Mavoko nje ya WCB anawatesa au anateseka ?

Tuesday August 13 2019

 

By Luqman Maloto na Dk Levy

DAKTARI Levy katoka alipotoka na ‘mistimu’ yake au sijui mlungula wa WCB, kaanza kumrukia ‘vifuti’ Rich Movoko. Ooh, si ndo akakutana na Luqman Maloto! Pamechimbika!

LEVY: Hata kama ukweli ni kwamba Rich Mavoko amepotea baada ya kuwatosa WCB, na Aslay mizuka imepungua. Nadhani kuna tatizo kwenye uongozi wake. Kwa maana yule dogo siyo wa kutoweka muda mrefu hivi.

LUQMAN: Leo umekula maharage ya wapi? Unaanza tu na hoja ambazo hata hazina link. Hebu niambie link ya Mavoko na Aslay ni nini?

LEVY: Kisanii ni kama wako dimbwini. Wamefubaa kama sare za askari wa Sudan Kusini. Yaani kama ni timu ya mpira basi ni RTC Kigoma au Mecco ya Mbeya huko.

LUQMAN: Rich Movoko si ndo mnamwita Messi wa Bongo Fleva, leo unasema amefubaa. Kweli Messi anaweza kufubaa?

LEVY: Kuondoka WCB ni jambo moja. Kuendelea kung’ara nje ya WCB ni jambo lingine na zito sana. Hivi huwa wanaondoka bila plan au wanakuwa wamerogwa?

Advertisement

LUQMAN: Kwani Mavoko alianzia muziki WCB? Mwache aendelee kuchanja mbuga nje ya WCB. Inaonekana huna taarifa sahihi. Unasema Aslay kafubaa wakati mtaani ngoma yake mpya “Chuki” inawashika mbaya.

LEVY: Mavoko wa kabla ya WCB hakuwa lolote ndo maama akajiunga ili arudi upya. Mavoko wa nje ya WCB hivi sasa ni tofauti na yule wa ndani ya WCB. Siku tukiacha kupeana moyo na kusimamia ukweli hili game litabadilika.

LUQMAN: Kati ya wewe na Mavoko nani alikuwepo WCB?

LEVY: Kwani muziki wanafanya kwa ajili ya mademu zao? Au kwa ajili ya dada zao? Muziki wao uko wazi na biashara ya muziki haina kificho. Tunaona. Tuache kupeana moyo tusiamamie ukweli ili game libadilike. Mavoko huyu siyo yule wa WCB. Muziki wa sasa hautegemei show wala mauzo ya ‘kaseti’, badala yake malipo ya YouTube kupitia ‘vyuuz’ ndo yanayowakalisha mjini. WCB ina wafuasi wengi sana ambao kazi yoyote ya WCB wao wanaipokea na kuishambulia ili ikimbize YouTube. Huko ndiko Mavoko alikotakiwa kuwaza. Nje ya WCB Mavoko hana base inayoeleweka. Vyovyote iwavyo labda mtuambie kuwa bado anajipanga. Lakini ngoma kadhaa alizotoa nje ya WCB sioni dalili njema mbele ya safari yake.

LUQMAN: Nimekuuliza swali, unakwepa. Mavoko alifanya muziki kabla ya WCB. Baadaye akaingia WCB. Chawa, kunguni, viroboto, sisimizi, mende, siafu, kila kitu anakijua. Akaona bora alipokuwa nje ya WCB, amejitoa. Hapo kuna shida gani arifu?

LEVY: Kwani Lowassa au Ajibu au Zitto hawakujua matatizo ya ndani ya vyama vyao? Lakini mbona tunawajadili? Ni kwa sababu shughuli zao zinaigusa jamii na jamii iliyoelimika inajua kinachoendelea. Hata biashara ya muziki ni ya kijamii. Kila kitu kipo wazi. Chawa

haohao. Viroboto hao hao. Kunguni na mende wa WCB ndo waliokuwa wanaingia YouTube kutazama ngoma zake na kupata namba kubwa ya ‘vyuuz’. Na sasa tunaona idadi ndogo ya ‘vyuuz’ akitoa ngoma.

LUQMAN: Mfano Mavoko anapata vyuuz za kumwagililu mpaka kusaza akiwa WCB lakini pesa haoni, halafu nje ya WCB akapata vyuuz chache na mpunga ukawa wa kutosha, hapo bora ni gani jombaa?

LEVY: Unajuaje kuwa alikuwa hapati mpunga wa kutosha? Okay sawa, kwa hiyo jibu ni kuondoka au kurekebisha mkataba ili kuweka sawa maslahi yake? Unapokuwa WCB usiwaze juu ya Diamond na Babu Tale. Anza kwanza kuwafikiria mamilioni ya mashabiki lialia wa WCB.

Wale ndo mtaji wenyewe na sio Sallam SK.

LUQMAN: Mwisho kabisa WCB ni duka la mtu. Lazima mwenye duka aangalie kwanza hesabu zake ndio wengine wafuate. Mimi sijawahi kuwepo WCB, hivyo sijui panya waliomo. Wanasema siri ya mtu anaijua kata!

LEVY: WCB usifananishe na duka la Mangi wa mtaani kwako. WCB ni brand ambayo kimsingi inasaidia na kukuwezesha msanii mwenye mashabiki watatu, kupata mashabiki mia moja. Sasa akili kichwani mwako. Kubaki na mashabiki watatu au kupata mashabiki thelathini kati ya mia moja utakaowapata kupitia WCB.

LUQMAN: Mwarabu Fighter alikuwa anang’ara WCB kwa sababu ya kuwa bodyguard wa Diamond, kumbe mshahara laki 5, na hakupewa miezi mitatu mpaka akakimbia njaa. Mpaka leo anadai. Kuna kipindi mwanaye aliumwa, akataka laki 3 za matibabu, hakuna mtu WCB alimpa. Aliomba apewe ili akatwe kwenye mshahara, akanyimwa. Tuwe ‘sirias’ Levy, tusubiri Mavoko alie ukata nje ya WCB ndio tumhukumu, ila kwa sasa, nasema hivi, kitanda usichokilalia hujui kunguni wake!

LEVY: Achana na misemo ya wahenga ambao ndio waliotufelisha mpaka leo. Kwa nini unatolea mifano ya walipofeli unaacha walipofaulu? Mwarabu Fighter anaingiaje kwenye suala la Mavoko? Mwarabu mbeba vyuma, Mavoko mwanamuziki. Unapomuongelea Mavoko tolea mifano skina Harmonize na wenzake. Huyo Mwarabu angalau ungemuingiza kwenye mfano huo kama mjadala ungekuwa unamuhusu Kifesi labda.

LUQMAN: Kwani mpaka Mavoko awe na demu Mzungu mwenye hela kama yule Sarah wa Harmonize ndio ujue yupo vizuri? Mavoko ndo ameshaondoka WCB sasa, wewe unataka nini?

LEVY: Dem Mzungu ataishi kama digidigi Mburahati huko sijui Kigogo Mbuyuni? Tatizo ninyi Wabongo vichwa maji sana. Nitajie msanii mkubwa wa kimataifa asiyekuwa na ‘lebo’. Huwezi kufanikiwa kwa kufanya muziki kibinafsi. Wote wanaotamba duniani pesa zao kuna mgawanyo mkubwa sana kutokana na uwepo wa mikono mingi. Na duni ya muziki ilivyo. Kutaka kufanya kila kitu peke yako ni kitaka kuishi dunia ya kale.

LUQMAN: Ni kweli kabisa, ndio maana Mavoko amekuja na lebo yake ya “Bilionea Kid”. Na yeye anataka kusimamia wasanii. Nadhani tumsapoti afike mbali, atoe ajira kama Diamond anavyofanya. Si kumng’ang’aniza aendelee kuuza duka la mwenzake, wakati naye uwezo wa kumiliki duka anao.

LEVY: Kuendelea kusema WCB ni duka la mtu ni uchonganishi na kuleta taswira mbaya kwa jamii. WCB ni zaidi ya duka. Hafaidiki Diamond pekee. Na hatuwezi kuwa watu wa kusapoti kila kitu tutakuwa hatujengi. Kwani Bongo Movie ilifeli wapi? Ni baada ya kila msanii kutaka kuwa ‘prodyuza’ yeye mwenyewe. Sasa unaongelea Bilionea Kid ndo nini? Ukweli ni kwamba Mavoko anahitaji kusukumwa ili apae zaidi kabla ya kuwaza kunyanyua wengine. WCB ni brand kubwa, angeweza kuwa na Bilionea Kid akiwa ndani ya WCB vilevile. Unaelewa nini unapoona video ya 50 Cent inapoanza au kuisha, chini kuna maandishi yameandikwa ‘lebo’ zaidi ya nne. Ni kwamba yeye mwenyewe anayo ‘lebo” yake, akiwa chini ya Eminem na Dr Dre.

Achana na kampuni la usambazaji wa kazi zake.

LUQMAN: Hata huyo 50 Cent mwenyewe alishaachana na Aftermath ya Dre na Shady ya Eminem, kazi zake zote anazifanya na lebo yake ya G-Unit. Hayo ndio maendeleo. Na Mavoko naye amekuja na Bilionea Kid. Kama inakutesa, teseka at your own risk. Unajua Levy huwa

sikuamini, kuna siku hapa Kijiweni ulimponda Kaseja lakini ndio huyo ametuvusha kwa Wakenya, tunazitafuta fainali za Chan. Kama uwezo wa kudaka penalti wa Kaseja unakutesa, teseka at your own risk!

LEVY: Yaani waswahili kila kitu cha zamani kilikuwa kizuri. Utasikia muziki zamani bana. Mpira wa enzi zetu bana. Siku hizi hakuna warembo kama zamani. Disco zamani pale Lang’ata, Mbowe, YMCA, Magoti na Agip ilikuwa babkubwa. Watangazaji wa mpira zamani nd’o walijua kutangaza akina Ahmed Jongo, Swed Mwinyi, Jumanne Mayoka, Salim Mbonde na kina Charles Hilalry. Bunge la zamani la kina Njelu Kasaka, lilileta mpaka G55. Lakini naona wewe nd’o kiumbe pekee unayepuuza maneno yangu ya zamani. Mimi nilimponda Manula wako na tabia yake ya kupangua mipira kama anadaka panzi. Kaseja nd’o kipa aliyestahili kumuongoza Manula. Sema siasa zenu za soka nd’o zinamponza. Tukiendelea kuwakumbuka wakongwe na wao wakitushangaza kama Kaseja. Sitashangaa kusikia Muhidim Aman Ndolanga na Ismail Aden Rage wakichukua nafasi pale TFF.

LUQMAN: Tatizo una maneno mengi kama vile ulichelewa kutembea. Uvivu wa kutembea huongeza ari ya mdomo. Leo unamsifu Kaseja kiaina. Sasa nijibu kati ya Wananchi Day na Simba Day nini hasahasa ndio Day?

LEVY: Nilishaapa kutoongelea siasa za Simba na Yanga. Wanaigana sana. Sasa achana na hilo, kumbe tajiri wa Simba naye njaa tu. Kaanzisha Kubwa Kuliko yake, ila yeye kaibadilisha jina anaiita Gal. Yaani kila mwaka wanachama wataichangia timu yao chochote

hata mlenda, mbaazi au kunde sawa tu. Hizi timu hazichekani. Kifupi ni kwamba Simba na Yanga ni maiti wanaotembea. Nakuacha na swali hili la msingi toka kwa ‘Komredi’ Kilomoni. MO ni mfadhili au mwanahisa? Hili ni swali kubwa saana ila watu hawaelewi!

Advertisement