Redknapp amfagilia Kane

Muktasari:

Redknapp ampongeza nahodha wa Tottenham, Harry Kane, kwa kuifungia timu yake mabao yote  muhimu katika ushindi wa 2-1 dhidi ya PSV ya Uholanzi, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Wembley.

London, England. Gwiji la soka nchini Uingereza, Harry Redknapp amemfagilia nahodha wa Tottenhma, Harry Kane kwa kuwaongoza wenzake kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mchezo huo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Wembley, wenyeji walifungwa bao la mapema na PSV dakika ya pili likiwekwa wavuni na De Jong, lililodumu hadi mapumziko.

Hata hivyo Kane mmoja wa washambuliaji mahiri wa Uingereza kwa sasa, aliirudisha Tottenham mchezoni alipofunga bao la kusawazisha dakika ya 78 kabla ya kufunga la ushindi dakika ya 89.

Redknapp, ambaye alipata kumnoa Kane kwa miaka mitatu wakati akiifundisha Spusr alisema mshambuliaji huyo amethibitisha ubora, thamani na umuhimu wake kama nahodha ndani ya kikosi.

“Kwa kweli Kane amethibitisha umuhimu wake kama nahodha, ametimiza wajibu wake kwa kiwango cha juu kabisa, alipofunga bao la kwanza aliitoa timu katika matatizo na bao lake la ushindi limefrudisha matumaini upya, ninampongeza kwa kuwa mfano bora,” alisema.

Naye Kocha wa timu hiyo, Mauricio Pochettino aliungana na Redknapp kumpongeza Kane akisema sasa amepata matumaini mapya ya kufuzu kwa hatua ya 16 bora.

Spurs yenye pointi nne ikifanikiwa kushinda mechi zake mbili zilizosalia itafikisha pointi kumi na kuungana na Barcelona kutinga hatua ya 16 bora kutoka kundi B.