VIDEO: Rasmi Yanga yampa Farid miaka miwili

Muktasari:

Winga Farid Mussa amerejea nchini kwa ajili ya msimu ujao kuitumikia Yanga akitokea Tenerife ya Hispania baada ya kusaini miaka miwili kuitumikia klabu hiyo kongwe nchini.

Yanga imeendelea kukisuka kikosi chake baada ya leo kumalizana na winga wa kushoto Farid Mussa aliyesaini mkataba wa miaka miwili.

Mussa ambaye ni winga wa zamani wa Azam FC ametua Yanga akitokea Tenerife ya Hispania iliyokuwa imemchukua akitokea klabu hiyo ya matajiri wa Chamazi.

Usajili huo wa Mussa sasa ni rasmi anakuja kuziba nafasi ya Mnyarwanda Patrick Sibomana ambaye alisitishiwa mkatabana Yanga mara baada ya msimu uliomalizika kumalizika.

Winga huyo amesaini mkataba huo mbele ya Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM mhandisi Hersi Said ambao mbali na kuidhamini klabu hiyo pia imeamua kusimamia usajili katika kukiboresha kikosi cha Yanga.

Usajili huo wa Mussa sasa unamfanya kuwa nyota wa nane kusajiliwa na Yanga msimu huu akitanguliwa na kiungo Zawadi Mauya (Kagera Sugar), mabeki Bakari Mwamnyeto (Coastal Union), Yassin Mustapha (Polisi Tanzania).

Wengine ni mabeki Kibwana Shomari (Mtibwa Sugar), Abdallah Shaibu (Ninja), washambuliaji Waziri Junior (Mbao) na Yacouba Sogne (Asante Kotoko) huku kiungo Feisal Salum naye akiongezewa mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo.