Rashid Juma afunguka Simba ilivyomuibua akiuza karanga, mihogo mtaani

Wednesday June 26 2019

 

By Thobias Sebastian na Olipa Assa

WINGA Rashid Juma amefanya makubwa sana msimu uliomalizika.

Licha ya umri mdogo na uchanga wake katika soka, Juma amekinukisha hadi huko kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo ni ndoto ya takriban kila mwanasoka wa Bongo.

Kwa kijana ambaye miaka michache tu nyuma alikuwa mitaani akiuza karanga, mihogo na hata kubeba mizigo ili kusaidia familia, ni zaidi ya ndoto kuwa katika klabu kubwa kama ya Simba na zaidi kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya kukulia katika mazingira ya familia ya kipato cha chini yaliyomsukuma kuingia mtaani kupambana kusaidia mahitaji ya familia, Juma hakuwahi kukata tamaa.

Imani yake kwamba Mungu yupo na hamtupi mja wake, ilimfanya Juma kuongeza juhudi na sasa yuko katika kikosi kimoja na nyota wakubwa wa Ligi Kuu ya Bara kama Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi.

Mwanaspoti ambalo limekuwa likiongoza kwa kuwatangaza nyota wa Bongo, lilimsaka Juma ili kupata mawili matatu na kujenga hamasa kwa vijana wengine wa Kitanzania wakiwamo wanaoishi katika mazingira magumu kutokata tamaa ya maisha.

Advertisement

Kijana mwenye haiba ya aibu anayejitambulisha kama “Mtoto wa uswazi mwenye njaa ya mafanikio”, Juma aliwakaribisha waandishi wa Mwanaspoti nyumbani kwao Vikindu jijini Dar es Salaam kwa bashasha kubwa, akisema: “Karibuni uswahilini kwetu.”

Mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea huku lengo la Mwanaspoti likiwa ni kujua maisha yake nje ya uwanja na hatua ambayo ameanza kuipiga akiwa na Simba.

Mwanaspoti: Habari za mapumziko Rashid vipi za mtaani kwako?

Juma: Salama karibuni sana, nimefurahia ujio wenu kwani mtajua uhalisia wangu wa nilipotoka, naishije nikiwa mtaani na mengi mtakayotaka kuyajua kutoka kwangu.

Mwanaspoti: Nyumbani unapenda kufanya nini?

Juma: Nikiwa nyumbani nakuwa mtu wa kawaida kwani tangu nikiwa mdogo sina mambo mengi kwa sababu ni mtu wa uswahilini, huku ni sherehe muda wote kwani nakuwa karibu ndugu jamaa, marafiki na familia yangu.

Ila nikiwa nyumbani kama hivi ligi imemalizika huwa natumia muda wangu mwingi kuwa nyumbani si mtu wa mitoko mingi.

Mwanaspoti: Kazi gani za nyumbani unapenda kufanya?

Juma: Nikiwa nyumbani nakuwa sina mambo mengi kama nilivyosema hapo awali, natumia muda wangu kufanya kazi za nyumbani kama kufua nguo zangu, naosha vyombo ambavyo vitakuwa vimetumika na muda mwingine nafagia ndani na nje.

Mwanaspoti: Baada ya kupata umaarufu, watu wa mtaani kwako wanakuchukuliaje?

Juma: Unajua zamani kabla sijafahamika kuna mtu mlikuwa hamsalimiani pengine kutokana na tofauti zetu na ilikuwa mkikutana popote mnapitana tu, lakini sasa hivi mkikutana na ukampita kama zamani wanasambaza maneno kwa watu kuwa Juma anaringa na anajisikia tangu ameanza kucheza Simba.

Juma: Mwanzo hapa mtaani nilikuwa na uwezo wa kuingia kokote kula na kununua kitu chochote, lakini sasa hivi imekuwa ngumu na nashindwa kuwa huru kama zamani na muda wote nakuwa nyumbani nimejifungia mazingira ya ndani.

Mwanaspoti: Ukiwa nyumbani unapika chakula?

Juma: Niseme ukweli, katika kitu ambacho sina utaalam nacho wala sifahamu ni kupika na siku zote nakula chakula ambacho kimepikwa na mtu mwingine. Ikitokea hakuna mtu wa kupika huwa naenda kununua.

Hata hili la kuosha vyombo lilikuwa changamoto kwangu ingawa sasa hivi napambana nalo na nitajitahidi kuzoea na kuliweza kabisa.

Mwanaspoti: Watu maarufu huwa wanakumbana na vishawishi vya kufuatwa na wasichana, kwa upande wako likoje?

Juma: Tangu zamani nikiwa mdogo nilikuwa sina mambo mengi ya wanawake, ingawa tangu nimekuwa maarufu nimekuwa na nyota ya kufuatwa na wasichana wengi hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Lakini wasichana wanaonifahamu wengi wananiogopa kwani nimekuwa mkali na wala sitaki mazoea nao bora hata hapo zamani nilikuwa mkarimu kidogo.

Nimeamua kuwa mkali kama njia ya kuwakwepa kwani bila ya kufanya hivyo naweza kupoteza miiko ya kazi yangu kwasababu haitaki hayo mambo hata kidogo na kama nikiwa nafanya nitashindwa kutimiza malengo yangu ya kufika mbali.

Mwanaspoti: Unarudisha vipi kwa jamii kile unachopata?

Juma: Bado sijafanikiwa katika mpira kwani ndiyo kwanza nimeanza. Kwa maana hiyo kufanya vitu vikubwa ni ngumu, lakini nimekuwa nikiwapa baadhi ya vifaa wachezaji mpira wengi wa mtaani kwangu.

Miongoni mwa malengo niliyonayo kama nitafanikiwa zaidi katika soka, sitawasahau ndugu na jamaa zangu wote ambao nipo nao hapa mtaani kwani kila mmoja ana mchango wake na bila wao pengine nisingefika hapa.

Mwanaspoti: Ni jambo gani ambalo hautalisahau?

Juma: Kiukweli nimekutana na matukio mengi, lakini nakumbuka mwaka 2015, nilikodishwa (ndondo), na kwenda kucheza mechi ya fainali na timu moja ya Vikindu, ilikuwa Machimbi tena mabondeni kule ambako hata watu kupita ni wachache. Timu yangu ya Goroka FC, ilishinda lakini tuliowafunga walianzisha vurugu na hata zawadi za mabingwa zilishindwa kutolewa na ugomvi huo haukiishia hapo kwani wapinzani walikuja mpaka nyumbani kufanya vurugu kila siku kama mwezi mzima.

Mtaani kukawa hamna amani, kila familia ilikuwa inajifungia ndani. Tukaona haiwezekani. Katika kuhakikisha tunaliondoa hilo tuliamua kuweka ulinzi na tulipambana nao mpaka wakaamua kuacha. Hii inabaki katika kumbukumbu yangu kama ugomvi ambao ulitokana na mpira tena mbali lakini ukahamia mtaani.

Usikose sehemu ya mwisho keshokutwa uone supastaa wa Simba alivyookoa kipaji cha Juma uswazi huko. Unajua ilikuwaje?

Advertisement