Rashford hatihati kuivaa Liverpool, Solskjaer ajuta kumpanga

Muktasari:

Mshambuliajii huyo wa kimataifa wa England amekuwa tegemeo la Man United akiwa amefunga mabao 22 msimu huu.

London, England. Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema anajutia uamuzi wake wa kumchezesha Marcus Rashford baada ya mshambuliaji huyo kuumia mgongo.

Rashford (22), alitolewa dakika 80 akiwa amedumu uwanjani kwa dakika 16 tu tangu ameingia Manchester United ikishinda bao 1-0 dhidi ya Wolves katika mchezo wa marudiano wa Kombe la FA.

Mshambuliajii huyo wa kimataifa wa England amekuwa tegemeo la Man United akiwa amefunga mabao 22 msimu huu.

‘Tutampima kujua ukubwa wa tatizo lake kabla ya kuamua kama atacheza au vinginevyo. Kwa kweli sikupanga kumtumia, alikuwa na maumivu ya goti au la, lakini alipambana,”alisema Solskjaer.

Kocha huyo alisema amecheza kamari kumpanga Rashford katika mchezo huo, lakini jambo la kufurahisha  alichangia matokeo mazuri ya Man United.

Alisema Rashford alicheza kwa ufanisi licha ya kucheza kwa tahadhari akihofia kupata maumivu zaidi kutokana na jeraha alilokuwa nalo awali.

Rashford amecheza mechi 13 kati ya hizo akianza katika michezo 11 na amekuwa chachu ya mafanikio katika kikosi hicho.