Raptors bingwa mpya NBA, wana rekodi tamu

Muktasari:

  • Hii ni mara ya kwanza kwa ligi hiyo maarufu zaidi Duniani bingwa wake anatokea nje ya Marekani.

Dodoma. We the North sasa ni ‘We the Champions!’, hiyo ni baada ya Toronto Raptors kufanikiwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani (NBA).

Raptors wameibuka mabingwa wapya wa ligi hiyo kwa ushindi wa pointi 110-114 dhidi ya wapinzani wao Golden State Warriors, mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Oracle Arena uliopo Oakland California.

Ushindi huo umeifanya Toronto Raptors kuibuka na ushindi wa jumla wa 4-2 dhidi ya Golden State Warriors na kuwa timu ya kwanza kutoka nchini Canada na nje ya Marekani kushinda ubingwa huo.

Sio hilo tu, Raptors pia haijawahi kufika fainali ya ligi hiyo tangu walipoingia kwa mara ya kwanza ligi hiyo mwaka 1995.

 

Kabla ya ushindi huo, timu za Canada hazijawahi kuwa na cha kujivunia kwani mara zote huishia katika mashindano madogo. Taji la Raptors limemaliza nuksi ya timu za Canada kuendelea kuwa wasindikizaji, ambapo mara ya mwisho ilikuwa miaka 26 iliyopita (1993) pale Toronto Blue Jays iliposhinda taji ambalo hata hivyo si la NBA.

Katika ushindi huo, Nyota Kyle Lowry na Mcameroon Pascal Siakam wote wawili walifunga pointi 26 kila mmoja wakiongoza kwa pointi ikiwemo Ribaundi 10 za Siakam na Asisti 10 pia za Lowry.

Upande wa Golden State Warriors, nyota Klay Thompson aliongoza kwa pointi zake 30 licha ya kushindwa kuendelea na mchezo dakika mbili za mwisho za robo ya kwanza katika kipindi cha pili akiumia mguu wa kushoto.

Kuumia kwa Klay ilikuwa pigo kubwa kwa Warriors kutokana na nyota huyo kutarajiwa kuamua mchezo wa leo baada ya kuwa na mchezo bora kabla ya kuumia baada ya nyota Steph Curry kudhibitiwa akifunga pointi 21 pekee.

Klay aliendeleza majanga kwa Warriors kufuatia kuumia kwake katika mchezo muhimu baada ya mchezo uliopita nyota mwingine Kevin Durant kuumia na kuipa pigo timu hiyo kujaribu kupindua matokeo ya 3-1.

Wachezaji wengine wa Warriors, Andre Iguodala alifunga pointi 22 wakati Draymond Green akitisha kwa kufunga pointi 11, ribaundi 18 na asisti 13.

Kwa matokeo hayo, Golden State Warriors wameshindwa kuendeleza ubabe waliokuwa nao ambapo walikuwa wametwaa taji hilo mara tatu ndani ya misimu minne iliyopita na walikuwa wanajaribu kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo.

KAWHI ABEBA TUZO YA MVP 

Amevuna alichopanda!, Nyota Kawhi Leonard amefanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji mwenye thamani zaidi (MVP) wa mechi za fainali hiyo.

Katika mchezo wa mwisho leo alifunga pointi 22 pekee tofauti na mechi zilizopita na ribaundi sita na asisti tatu ikiwemo pointi zake za mwishoni zilizoihakikishia Raptors ushindi leo.

Tuzo hiyo ni ya pili kwake baada ya awali kutwaa mwaka 2014 akiwa na San Antonio Spurs ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwa timu hiyo akitokea kubadilishwa na DeMar DeRozan aliyeenda Spurs.